Kenya hatimaye yapokea chanjo ya corona
3 Machi 2021Wakati huo huo, baraza la magavana limetoa wito kwa Rais Uhuru Kenyatta kuongoza katika kupokea chanjo hiyo ili kuondoa hofu kwa wananchi ambao wana shaka nayo.
Juhudi za kupambana na virusi vya corona, zimepigwa jeki baada ya Waziri wa Afya nchini Kenya Mutahi Kagwe kuongoza hafla ya kupokea shehena ya chanjo katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Jommo Kenyatta.
Chanjo hizo zilisafirishwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Watoto-UNICEF kama sehemu ya mpango wa COVAX, unaolenga kununua na kusambaza chanjo za bure kwa nchi maskini zaidi duniani.
Umma utaendelea kuhamasishwa kuhusiana na chanjo
Waziri Kagwe amesema kuwasili kwa shehena hiyo ni historia kwa taifa la Kenya na kwamba zitahifadhiwa kwenye mazingira baridi.
"Tutaendelea kuuhamasisha umma kuhusu mchakato mzima wa chanjo zitakapoanza kutolewa. Chanjo si jambo geni Kenya,” alisema waziri Kagwe.
Wizara ya Afya imeweka mpango wa kusambaza chanjo hizo kwenye kaunti zote 47 huku wafanyakazi walio kwenye mstari wa mbele katika vita hivyo wakipewa kipaumbele cha kupokea chanjo hiyo.
Chanjo hizo zitasafirishwa katika vituo tisa ambapo majimbo yatapata fursa ya kuchukua na kusambaza kwenye hospitali. Hospitali za rufaa ndizo zitakazopewa kipaumbele pamoja na hospitali binafsi zilizochaguliwa.
Watakaopokea chanjo hiyo watapata mara mbili kwa kipindi cha majuma manane. Dokta Willis Akhwale anayeongoza jopokazi linaloshughulikia chanjo hiyo, anafafanua zaidi.
"Katika siku mbili au tatu, chanjo zitakuwa zimewasilishwa katika vituo vikuu vya maeneo. Majimbo yanaweza kuzipokea. Majimbo yaliyoko karibu ya Nairobi, yataanza kutoa chanjo mwishoni mwa wiki,” alisema Akhwale.
Mataifa 10 ya Afrika tayari yameanza mchakato wa kuwachanja raia wake
Wakati huo huo, baraza la magavana limetoa wito kwa uongozi wa taifa kuonesha kwa vitendo na kupokea chanjo hiyo mbele ya umma. Baraza hilo limedai kuwa, Wakenya wengi wana hofu kuhusu chanjo hiyo na kwamba hatua hiyo itawaondolea hofu wananchi.
Kenya sasa inajiunga na mataifa ya Ghana, Ivory Coast na Nigeria ambayo yameshapokea shehena zao za chanjo ya COVID-19. Karibu mataifa 10 ya Afrika yameanza kuwachanja wananchi wake. Mataifa hayo ni pamoja na Afrika Kusini, Ivory Coast, Ghana, Zimbabwe, Senegal, Morocco na Misri.
Hadi kufikia sasa Kenya imerekodi visa 106,470 vya virusi vya corona tangu mwezi Machi mwaka 2020, huku watu 1,863 wakiwa wamefariki dunia.