Kenya inavyopambana kuwalinda watumiaji wa mitandao
7 Februari 2024Akisimulia tukio la mauaji ya mwanafunzi aliyehadaiwa mtandaoni, ambalo wamekuwa wakilifanyia uchunguzi, Kamisha wa Kaunti ya Nakuru, Lyford Kibaara, anasema ukosefu wa usalama kwa watoto na vijana kwenye mtandao ni hali inayotia wasiwasi.
Yisa vingi vya unyanyasaji mtandaoni vinachangiwa na upatikanaji rahisi wa maudhui ya picha za ngono, ulaghai wa mtandaoni na uingiliaji wa masuala ya faragha.
Soma zaidi: Kenya yawaonya watumiaji wa mitandao ya kijamii
“Unasikia huyo mtoto akisema walikutana kwenye mtandao. Ni mtu ambaye hamjui. Na wakati mmoja anamuuliza, wewe unaniita unataka kuniua, yule anamuuliza unafikiria nitakuua kwa nini? Hawa watoto wetu - hata wale wachanga - wanajua mambo ya mtandao hata kutushinda sisi. Sisi kama wazazi tumejikuta hatuwajibiki vilivyo katika majukumu yetu ya kulea watoto.” Anasema Kibaara.
Wizara ya elimu nchini Kenya imetakiwa kutengeneza mifumo ya masomo ya uhamasishaji kwa watoto kuhusu mitandao na kuwatahadharisha kuhusu usalama wao kwenye mtandao.
Mchango wa elimu
Walimu, wazazi na maafisa wa usalama wana jukumu kubwa la kutengeneza mazingira bora kwa watoto wanaotumia huduma za mtandao.
Watoto wengi wamekuwa wakitumia muda mwingi mtandaoni hasa baada ya mabadiliko yaliyoletwa na janga la UVIKO-19 yaliyowezesha mfumo wa kujifunza kupitia njia ya mtandao.
Hali hii imeongeza visa vya unyanyasaji mtandaoni na uraibu wa mtandao kwa kundi la vijana.
Wizara ya mipango maalum pamoja na washirika wa kitaifa na kimataifa imezindua taratibu za uendeshaji wa shughuli za kudhibiti dhuluma na unyanyasaji wa kingono kwa watoto mtandaoni nchini Kenya.
“Tumepitisha sera yetu ya ulezi wa Watoto ambayo pia tunaileta kwenye jamii, ili itusaidie kuhakikisha ya kwamba tumekuza jamii zetu kwa maadili ambayo ni bora.” Anasema Joseph Motari, katibu mkuu katika wizara ya mipango maalum, akiongeza kuwa ni muhimu kuzingatia na kuwekeza katika usalama wa watoto mtandaoni ili kuwasaidia kunufaika na faida za mtandao.
Mchango wa mashirika na asasi
Watungaji sera wametakiwa kupigia debe mifumo inayohakikisha teknolojia inayozingatia haki za kibinadamu, haki ya faragha na uhuru wa kujieleza na afya ya kiakili.
Alice Anokur, mkurugenzi wa shirika la kimataifa la Child Fund nchini Kenya, alisema asilimia 67 ya watoto nchini Kenya wanatumia mtandao, ikimaanisha kwamba wanau wezo wa kuona maudhui mazuri na yasiyowafaa.
Alisema wanafanya kazi katika shule 60 nchini Kenya kuwapa watoto muongozo mzuri wa utumiaji wa mtandao.
“Tunataka kuwafikia Watoto, kuwalinda na kuwafahamisha kwamba kuna maudhui mabaya ambayo hawapaswi kuyafuata mtandaoni. Watumie mtandao kwa ajili ya masomo, kujifunza mambo mazuri na sio yanayowadhuru.” Aliongeza.
Huku upatikanaji wa huduma za intaneti ukiendelea kuimarika barani Afrika, huduma ya mtandao nchini Kenya imeorodheshwa miongoni mwa zile zinazofanya vizuri zaidi barani Afrika, Afrika Kusini ikiongoza, kulingana na ripoti ya GSMA, ambalo ni shirika la kimataifa linalounganisha mfumo wa mawasiliano ya simu.
Imetayarishwa na Wakio Mbogho/DW Nakuru