1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya kuzindua satelaiti mpya ya Taifa-1

5 Aprili 2023

Kenya itazindua satelaiti yake ya kwanza wiki ijayo. Hilo ni tukio la kihistoria kwenye programu ya usafiri wa anga nchini humo. Hii ni kwa mujibu wa serikali ya Kenya iliyotangaza mafanikio hayo siku ya Jumatatu.

https://p.dw.com/p/4Phw4
USA Raumfahrt l SpaceX Falcon 9-Rakete mit SWOT-Satelliten der NASA
Picha: Patrick T. Fallon/AFP

Satelaiti hiyo inayoitwa Taifa-1 itazinduliwa katika kituo cha usafiri wa anga cha Vandenberg jijini Carlifonia, Marekani mnamo Aprili 10 ambapo roketi ya SpaceX aina ya Falcon-9 ndio itatumika katika uzinduzi huo wa Satelaiti ya Kenya, Taifa-1.

Kwa mujibu wa Wizara ya Ulinzi na Shirika la Anga la Kenya, dhamira hii ni hatua muhimu na itachangia pakubwa kustawisha uchumi unaotokana na utafiti wa angani unaostawi nchini humo.

Satelaiti hiyo itakayotumiwa kwa ajili ya kukusanya data juu ya utafiti wa kilimo na uhakika wa upatikanaji wa chakula imebuniwa na kutengenezwa na wahandisi wa Kenya.

Majaribio na utengenezaji wa vifaa vya satelaiti hiyo ulifanyika kwa ushirikiano na kampuni ya Bulgaria inayoshughulikia utafiti wa anga.

Kenya ambayo ni injini ya uchumi kwenye eneo la Afrika Mashariki inakabiliwa na ukame mkubwa kwa miongo kadhaa kutokana na mvua kukosa kunyesha vizuri kwa misimu mitano.

Uzinduzi huo unayahamasisha mataifa ya Afrika ili kuongeza juhudi katika uvumbuzi wa kisayansi na maendeleo ya program za utafiti wa anga.

Misri ni nchi ya kwanza barani Afrika kupeleka satelaiti angani. Nchi hiyo ilizindua satelaiti yake mnamo mwaka 1998.

Kenya ilizindua satelaiti ndogo ya majaribio mwaka wa 2018 katika kituo cha anga cha kimataifa.

Kufikia mwaka wa 2022 takriban mataifa 13 ya kiafrika yalikua yametengeneza satelaiti 48 kwa mujibu wa kampuni ya Space in Africa ya Nigeria inayofuatilia harakati za utafiti wa anga barani Afrika.

Kampuni hiyo ya Space in Africa imesema kufikia Novemba mwaka 2022, zaidi ya satelaiti 50 zilizinduliwa na mataifa ya kiafrika ijapokuwa zote hizo zimepelekwa angani kutokea nje ya bara la Afrika.

AFP
Daniel Muteti