1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya na Somalia zakubaliana kutatua mzozo wao

Admin.WagnerD6 Machi 2020

Kenya na Somalia zimekubaliana kusuluhisha mzozo uliotishia kuvuruga uhusiano kati yao. Rais Uhuru Kenyatta na mwezake wa Somalia Abdullahi Farmaajo wamekubaliana kuteua kamati ya kushughulikia viini vya mzozo huo.

https://p.dw.com/p/3YxjH
Kenia Nairobi Besuch Somalischer Präsident
Picha: Getty Images/AFP/S. Maina

Shinikizo kutoka kwa serikali ya Marekani huenda lilimlazimisha rais wa Somalia Mohamed Farmaajo kupunguza joto ambalo lilikuwa linatisha kusamabaratisha uhusiano na taifa la Kenya kwa mujibu wa duru. Siku mbili baada ya Nairobi kuituhumu Somalia kwa kukiuka mipaka yake, wanajeshi wake walipopigana katika ardhi yake, rais Farmaajo alimpigia simu rais Uhuru Kenyatta, kwa lengo la kutafuta suluhu. Maafisa wa serikali ya Kenya hawakuelezea tukio hilo, hata hivyo wanadiplomasia wakuu Nairobi wamethibitisha kuwa ni rais Farmaajo aliyempigia rais Kenyatta simu, akiomba mwafaka. Maafisa katika ikulu ya Mogadishu wamethibitisha mazungumzo hayo ya simu lakini hawakusema nani aliyeyaanzisha.

Kwenye mawasiliano hayo yao ya simu viongozi hao wawili walijadili umuhimu wa kushirikiana na kutafuta suluhu ya mzozo kwenye mpakana na usalama kwa ujumla katika kanda hii. Kwenye mtandao wa Twitter, ikulu ya Somalia imesema kuwa marais hao wawili walikubaliana kuwa usalama wa mataifa hayo una uhusiano wa moja kwa moja na kwamba chochote ambacho huenda kikasababisha kutokuelewana lazima kiepukwe. Mzozo huo umeathiri wakazi wa Mandera, huku shule zikifungwa na walimu kukimbilia usalama wao. Kithiki Kindure ni seneta nchini Kenya.

Somalia imesema kuwa itaunda kamati ya pamoja kuboresha mahusiano ya kidiplomasia na biashara kwa maslahi ya raia wa mataifa hayo. Kwa miezi kadhaa sasa, wanajeshi wa Somalia na jimbo la Jubbaland wamekuwa wakipanga kukabiliana, baada ya waziri wa zamani wa Jubba Abdirashid Janan kutoroka gerezani Somalia na kuingia Jubba na kisha akatorokea Kenya. Hata hivyo kwenye mkutano wa baraza la usalama ulioongozwa na rais Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi hivi karibuni, suala la waziri huyo mtoro halikujadiliwa.

Balazo wa Somalia katika Umoja wa Mataifa Abukar Dahir Osman ameituhumu Kenya kwa kukiuka uhuru wa Somali. Amesema kuwa mamlaka ya Kenya inamhifadhi Janaan, na kuunga mkono wanajeshi wa Jubbaland. Mahusiano kati ya Kenya hayajakuwa mazuri, mwaka uliopita Kenya ilizuia ndege zake kusafiri Somalia, huku Somalia ikielekea katika mahakama ya Kimataifa ikidai kuwa Kenya ilikuwa imenyakua eneolake la mpaka kwenye bahari ya Hindi.