1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vijana wanaougua saratani waongezeka, Kenya

28 Oktoba 2024

Idadi ya vijana wanaoumwa saratani nchini Kenya inazidi kuongezeka. Takwimu zinaonyesha karibu vijana laki moja, wanaugua ugonjwa huo. Wahudumu wa afya wamelihusisha ongezeko hili na kutozingatia lishe bora.

https://p.dw.com/p/4mJqJ
Uvutaji wa sigara
Uvutaji wa sigara ni moja ya visababishi vikuu vya saratani kwa kundi la vijana Picha: Gareth Fuller/empics/picture alliance

Rita Opondo, (23) aligundua kuwa anaugua saratani ya matiti alipofika kufanyiwa vipimo baada ya kuhisi uvimbe kwenye titi lake.

Baada ya vipimo hivyo, alipata mawazo mengi na hasa alipoelezwa kwamba atakatwa titi lake. Kama haitoshi, kizingiti kingine kilikuwa ni kuwaarifu ndugu zake ambao tayari walimpoteza mmoja wao kutokana na ugonjwa huu, mbali na gharama kubwa za matibabu.

Wahudumu wa afya wanasema kuna umuhimu mkubwa wa kuendesha uhamasishaji miongoni mwa vijana ikizingatiwa kundi hili la raia mara nyingi hawaamini kwamba wanaweza wakapata saratani, ugonjwa huu ukiwa ungali unahusishwa na watu walio na umri mkubwa.

Kulingana na muungano wa mashirika ya saratani nchini Kenya, takwimu za sasa za maradhi ya saratani miongoni mwa vijana ni virusi vya HPV vinavyosambazwa kwa ngono vikihusishwa na ongezeko hili wito ukitolewa kwa vijana kuwa makini katika mahusiano yao ya kimwili.

Soma pia:Mamilioni ya watu hatarini kukumbwa na maradhi kutokana na kutofanya mazoezi 

Papilloma virus (HPV)
Virusi vya ​​Papilloma vinavyosababisha saratani ya mlango wa kizaziPicha: Cavallini/BSIP/picture alliance

Uhamasishaji zaidi unahitajika

Rose Atieno kutoka Shirika la Afya For Africa anasema kando na uhamasishaji wa saratani mfano mwezi wa Oktoba kila mwaka ambapo uhamasishaji wa saratani ya matiti unaendelea, kuna haja ya kampeni zaidi kuendeshwa mitandaoni na katika taasisi za elimu kuanzia kiwango cha chini hadi juu.

Anahimiza umuhimu wa serikali kuimarisha mifumo ya hudumu ya afya katika kitengo cha saratanikusaidia kupunguza gharama na walioathirika kujiunga na makundi yatakayosaidia kutoa ushauri nasaha na kuhakikisha pia afya ya akili ya wahusika inasalia imara katika safari ya matibabu ya saratani.

"Saa zingine unakutana na mtu kutaka kumueleza kuhusu saratani na kuona ni vipi unaweza kumsaidia."

Tizama pia:

Vitu vinavyo chochea saratani

Kutafuta matibabu mapema kunasaidia pakubwa kupambana na kusambaa kwa maradhi haya na kuokoa maisha.