Kenya yamteua Balozi Amina Mohamed WTO
16 Januari 2013Balozi Amina ambaye anahudumu katika wadhifa wa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na vile vile Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) lililo na makao yake makuu mjini Nairobi alizindua kampeni yake jana jioni katika hoteli ya Intercontinental.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Kenya, Prof. Sam Ongeri, Waziri wa Biashara, Moses Wetangula, na maafisa wa kibalozi kutoka nchi mbali mbali za ulimwengu.
Balozi Amina ambaye kitaaluma ni wakili, amewahi kufanya kazi katika serikali ya Kenya akiwa mshauri wa kisheria katika wizara ya mambo ya nje. Amewahi kuwa Balozi wa Kenya katika Umoja wa Mataifa na amekuwa mwanachama wa bodi kuu na kamati za mashirika mbali mbali ya Umoja wa Mataifa.
Balozi Amina Mohammed ataaanza kampeni yake kwa kutembelea miji mikuu ya mataifa wanachama wa Shirika la WTO, ambayo itakampeleka hadi Geneva tarehe 30 mwezi huu ambapo atakutana na wagombea wenzake wanane wanaopigania nafasi hiyo.
Wagombea wengine wanaopigania nafasi hiyo ni; Alan John Kwadwo kutoka Ghana, Bi Anabel González wa Costa Rica, Bi Mari Elka Pangestu kutoka Indonesia, Tim Groser kutoka New Zealand, Ahmad Thougan Hindawi kutoka nchini Jordan, Herminio Blanco kutoka Mexico, Bwana Taeho Bark kutoka Jamuhuri ya Korea Na Roberto Carvalho de Azevêdo kutoka Brazil.
Amina anasema endapo atachaguliwa lengo lake kuu litakuwa kukabiliana na changamoto zinazokumba shirika la WTO ikiwa ni pamoja na mashauri ya kibiashara katika uchumi wa dunia.
Mwandishi: Alfred Kiti/DW Nairobi
Mhariri: Josephat Charo