1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yamwaga polisi kukabili wimbi jipya la maandamano

8 Agosti 2024

Polisi nchini Kenya wameshika doria leo katika maeneo ya mji mkuu Nairobi na katika miji mingine ya nchi hiyo kutokana na maandamano mapya ya kuipinga serikali.

https://p.dw.com/p/4jF1s
Maandamano ya umma nchini Kenya
Makabiliano kati ya polisi na waandamanaji mjini Nairobi.Picha: Thomas Mukoya/REUTERS

Vizuizi vimewekwa kwenye barabara kadhaa za Nairobi huku maduka mengi yakisalia kufungwa. Polisi imefyatua mabomu ya kutosha machozi kuyatawanya makundi madogo ya waandamanaji waliojitokeza Nairobi.

Taifa hilo la Afrika Mashariki limekumbwa na maandamano ya wiki kadhaa kwa kiasi kikubwa yakiongozwa na vijana, ambayo wakati mwingine yaligeuka kuwa ghasia.

Kaimu Inspekta Mkuu wa Polisi Gilbert Masengeli jana alionya kuwa watu aliowaita wahalifu walitaka kujiingiza katika maandamano hayo na akawataka Wakenya kujiepusha na maeneo yaliyopigwa marufuku kuingia bila ruhusa kama vile uwanja mkuu wa ndege na Ikulu ya Rais.

Vijana wanaoandamana wanadai uwajibikaji, mabadiliko na uongozi bora katika serikali ya sasa.

Wakati huo huo, Rais William Ruto ameliapisha mapema leo baraza lake jipya la mawaziri 19 katika Ikulu ya Nairobi. Baraza hilo linawajumuisha mawaziri kutoka vyama vya upinzani katika kile ambacho Ruto amesema ni serikali pana.