1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiKenya

Kenya yaondoa tozo kwa mkate kufuatia maandamano

19 Juni 2024

Serikali ya Kenya imefutilia mbali mipango ya kuongeza tozo kwa mkate, magari na bidhaa zinazoagizwa kutoka nje na kuufanyia marekebisho mswada wenye utata ambao umechochea maandamano nchini humo.

https://p.dw.com/p/4hDxd
William Ruto Kenya Kongamano la tabianchi Africa
Rais wa Kenya William RutoPicha: Khalil Senosi/AP/picture alliance

Ofisi ya Rais imesema imeondoa pia tozo mpya kwenye miamala ya simu, usafirishaji wa sukari na mafuta ya mboga.

Wabunge walitarajiwa jana kuujadili mswada huo mpya wa fedha japo mjadala huo umeahirishwa hadi leo, saa chache tu kabla ya ofisi ya rais kutangaza mabadiliko hayo.

Soma pia: Wanaharakati nchini Kenya wapinga ongezeko jipya la kodi 

Taifa hilo lenye uchumi mkubwa Afrika Mashariki limekabiliwa na mzozo juu ya kupanda kwa gharama ya maisha huku wakosoaji wakionya kuwa tozo hizo mpya zitawaongezea Wakenya mzigo mkubwa zaidi.

Mamia ya waandamanaji wengi wao vijana walikusanyika karibu na bunge kupinga tozo hizo mpya huku polisi wakitumia mabomu ya machozi kuwatawanya. Shirika la kutetea haki za binadamu la KNHCR limesema watu 335 wamekamatwa.