Kenya yatumbukia gizani kutokana na hitilafu ya umeme
11 Desemba 2023Ukatikaji huo umeme wa Jumapili ulianza majira ya saa mbili usiku na ulikuwa hitilafu ya tatu ya kitaifa ya usambazaji wa umeme ndani ya miezi mitatu iliyopita.
Miongoni mwa vituo muhimu vilivyoathiriwa ni Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi, pamoja na Uwanja wa ndege wa Eldoret, magharibi mwa Kenya, ambapo jenereta za dharura za umeme pia zilishindwa kuwaka baada ya gridi ya umeme kupata hitilafu.
Shirika la umeme la serikali, Kenya Power, limesema kukatika huko kwa umeme kumetokana na "mvurugiko kwenye mfumo" ambao lilidai kuwa ulikuwa ukishughulikiwa na mafundi.
"Tumepoteza ugavi wa umeme katika maeneo mbalimbali nchini kutokana na hitilafu inayoathiri mfumo wetu," ilisema taarifa. "Tunashughulika kurejesha hali ya kawaida katika muda mfupi iwezekanavyo."
Kampuni ya taifa ya Kenya Power inahodhi ugavi na usambazaji wa umeme, lakini kwa miaka kadhaa imelaumiwa kwa huduma duni na rushwa, ambavyo vimesababisha gharama kubwa ya umeme nchini Kenya.
Baadhi ya maeneo ya nchi yaliripoti kwamba umeme ulirejea baada ya saa mbili.
Waziri anayehusika na nishati, Davis Chirchir, alisema ukatijaji huo ulisababishwa na kuelemewa kwa njia ya kusafirisha umeme ya Kisumu-Muhoroni, ambayo ina uwezo wa kusafirisha MW 80 lakini ilikuwa inasifirisha MW 149.
"Hatujawezekeza sana kwenye mitandao. Tunapanga kukabidhi mitandao kadhaa ili iendelezwe na wawekezaji binafsi. Hii itapunguza shinikizo," alisema waziri Chirchir katika mkutano na waandishi habari mjini Nairobi siku ya Jumatatu.
Watumiaji wa mitandao wailinganisha Kenya Power na mashirika mabovu Afrika
Alibainisha kuwa kituo kipya cha kufua umeme na njia yenye urefu wa kilomita 90 vitapunguza mzigo kwenye njia ya Muhoroni-Kisumu. "Tutajenga laini mpya ya KV33 kati ya Narok na Bomet ili kuzuwia ukatikaji wa mara kwa mara wa umeme, na kuzuwia kuitumbukiza nchi katika giza," alisema waziri huyo wa nishati.
iliwachukulia wahandisi zaidi ya saa 12 kurejesha umeme katika maeneo mengi ya nchi. Lakini ukatikaji mbaya zaidi ulitokea Agosti 25, mrefu zaid katika historia ya Kenya.
Chanzo chake kinasalia kuwa kitendawili, huku kampuni ya umeme ikilaumu kushindwa kwa shamba kubwa zaidi la upepo Afrika, ambalo pia liliekeza lawama kwa gridi ya umeme.
Katika baadhi ya maeneo ya nchi, ikiwemo Nairobi, ilichukuwa karibu saa 24 kwa umeme kurudi. Wakenya kwenye mitandao ya kijamii walidai majibu kutoka Kenya Power kuhusiana na kukatika mara kwa mara kwa umeme, kufuatia tukio la Jumapili, huku wengine wakilidhihaki shirika hilo, wakisema lilikuwa baya kuliko makampuni nchini Nigeria na Afrika Kusini, ambako mgao wa umeme ni jambo la kawaida.
Ukatikaji wa karibuni nchini Kenya unakuja wakati nchi hiyo inakabiliwa na bei za juu za nishati ya mafuta, ambazo wengi wamezilaumu kwa hasara ya mamilioni ya dola kwa bishara na uchumi jumla, unaopambana vibaya.