1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenyatta: Nitaendeleza kampeni dhidi ya ICC

8 Aprili 2016

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amesema anataka kuendelea na kampeni yake ya kuifanyia mageuzi Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu-ICC ya The Hague, Uholanzi.

https://p.dw.com/p/1IRrb
Deutschland Uhuru Kenyatta in Berlin
Picha: picture-alliance/dpa/B.v. Jutrczenka

Kauli hiyo ameitoa katika mahojiano maalum aliyofanyiwa na mwandishi wa DW, Daniel Pelz wakati wa ziara yake nchini Ujerumani. Alipoulizwa kama amezungumza na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel kuhusu kampeni yake ya kutaka mageuzi dhidi ya ICC au nchi za Afrika zijiondoe katika mahakama hiyo, Rais Kenyatta amesema hawakuligusia kabisa suala hilo. Amesema suala hilo halikuwa katika ajenda ya kuzungumzwa kwenye ziara yake ya sasa barani Ulaya.

Kuhusu hatua ya kuungwa mkono na nchi kama vile Ujerumani na Ufaransa katika mchakato wa mageuzi hayo ya ICC, Rais Kenyatta amesema wanashinikiza na kuelezea kwa ufasaha kuhusu kesi yao kupitia nchi zilizosaini Mkataba wa Roma uliyoianzisha mahakama hiyo na kupitia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambavyo ni vyombo muhimu kwa Kenya kushinikiza hoja yao.

Msimamo wa Kenya kuhusu ICC

Amesema wameelezea msimamo wao kuhusu mageuzi ya ICC kwa uwazi na wataendelea kufanya hivyo. Alipoulizwa kuhusu msimamo wa Kenya kama inataka mageuzi ya ICC au wanakubaliana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Louise Mushikiwabo, ambaye aliiambia DW kwamba ni bora nchi za Afrika ziondoke ICC, Rais Kenyatta alikuwa na haya ya kusema.

''Tunataka mageuzi, lakini pia tumejiandaa kuondoka ICC iwapo hatutafanikiwa kupata mageuzi muhimu tunayohitaji. Tunaiona mahakama hiyo kama isiyotekeleza mamlaka yake kama ilivyopaswa kufanya hivyo, wakati mkataba wa Roma ulivyoanzishwa kwa mara ya kwanza,'' alisema Kenyatta.

Kansela Angela Merkel na Rais Uhuru Kenyatta
Kansela Angela Merkel na Rais Uhuru KenyattaPicha: Reuters/H. Hanschke

Pia Rais Kenyatta amezungumzia kuhusu wawekazaji wa Kijerumani ambapo amesema ni eneo muhimu la ziara yake kwa sababu anaamini Kenya ina uhusiano imara na Ujerumani. Amesema tayari kuna idadi kubwa ya makampuni ya Kijerumani yaliyowekeza Kenya na yanafanya biashara nzuri kabisa nchini humo, ingawa wanataka idadi hiyo iongezeke.

Katika suala la rushwa iliyokithiri, ambalo wawekezaji wengi wa Kijerumani wana wasiwasi nalo, kiongozi huyo wa Kenya amesema nchi yake inasonga mbele haraka katika suala la kuleta mageuzi kwenye biashara.

Amesema wanalichukulia suala la rushwa kwa umakini mkubwa, kwani wanaimarisha sheria na kuanzisha muswada mpya unaomuhusu mtoaji na mpokeaji rushwa. Aidha, amebainisha kwamba baadhi ya mawaziri na watumishi wa umma kadhaa wamekamatwa.

Mahojiano hayo yalihitimishwa kwa kuzungumzia kitisho cha wanamgambo wa Al-Shabaab, ambapo Rais Kenyatta amesema ugaidi sio vita vya kitaifa, bali vya kimataifa.

Amesema wanahitaji msaada na ushirikiano mkubwa kutoka Ujerumani na Ulaya kwa ujumla, kwenye maeneo kama ya kupeana taarifa za kijasusi, kupambana na itikadi kali na kukabiliana na chanzo cha siasa kali.

Mwandishi: Daniel Pelz
Tafisiri: Grace Patricia Kabogo
Mhariri: Iddi Ssessanga