1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kerry afanya mazungumzo kwa siku tatu Mfululizo

mjahida4 Januari 2014

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry leo (04.01.2014) anatarajiwa kuwa na mazungumzo kwa siku ya tatu mfululizo na viongozi wa Israel na Palestina kujaribu kutafuta muongozo wa majadiliano ya mpango wa amani.

https://p.dw.com/p/1Al9f
US-Außenminister Kerry in Israel mit Premierminister Netanjahu 02.01.2014
Waziri John Kerry na Benjamin NetanyahuPicha: Brendan Smialowski/AFP/Getty Images

Baada ya zaidi ya saa nane ya mazungumzo siku ya Alhamisi na Ijumaa, Kerry atakutana tena na waziri mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu akitafuta mpango wa kuongoza majadiliano kuelekea katika amani kati ya pande hizo mbili.

Lakini maafisa wa Marekani walioonya hapo awali kwamba hawatarajii maafikiano ya haraka kuwepo wiki hii, wamekubali mpango huo wa amani utachukua muda kupatikana.

Kerry alikutana na rais wa Palestina Mahmood Abbas kwa saa sita siku ya Ijumaa ana anatarajiwa kufanya tena mazungumzo naye hii leo katika makao yake makuu katika ukingo wa Magharii.

John McCain bei Rede in St. Paul
Seneta John Mc CainPicha: AP

Hata hivyo pande zote mbili Israeli na Palestina zimeonesha kurudi nyuma kwao katika mpango uliopendekezwa na Kerry hata baada ya kuukubali mwezi Julai wakati mazungumzo ya moja kwa moja yalipoanzishwa tena baada ya kukwama kwa siku nyingi.

Kulingana na seneta John McCain wa chama cha Repablikan nchini Marekani, Waisraeli wana wasiwasi mkubwa juu ya usalama wao, iwapo mipaka yao itakuwa maeneo ambayo yatakuwa yanadhibitiwa na Wapalestina.

Kwa upande wake afisa wa ngazi ya juu wa Palestina Yasser Abed Rabbo siku ya Alhamisi alikuwa na shaka juu ya mpango huo wa amani akisema kwamba unaweka mipaka dhidi ya uhuru wa Palestina katika ukingo wa Magharibi.

Kerry asema mchakato mzima ni mgumu

Hata hivyo Waziri John Kerry amekiri mchakato mzima ni mgumu, lakini akasema kila siku wanapiga hatua muhimu. Kando na hilo afisa mmoja aliyekaribu na waziri mkuu wa Palestina Mahmoud Abbas ametupilia mbali mpango wa Kerry kwa kupendelea upande wa Israel.

Netanyahu siku ya alhamisi alionekana kumshambulia Abbas." Najua umejitolea katika kupatikana kwa amani na mimi najua nimejitolea kwa kupatikana amani lakini kwa bahari mbaya kutokana na maneno ya kiongozi wa Palestina, kuna shaka iwapo Israel kweli Wapalestina wamejitolea kutakia amani," Alisema Netanyahu.

kufuatia suala la kuachiwa kwa wafugwa wa Palestina nchini Israel kama mpango wa kuendelea kwa mazungumzo hayo, Netanyahu amesema kuwa Abbas anawaona magaidi kama mashujaa akisema suala hilo halikubaliki.

US Außenminister John Kerry und Palästinenser Präsident Mahmoud Abbas
Waziri Kerry na Rais Mahmood AbbasPicha: Reuters

Kerry amesema yuko tayari kufanya kazi na pande zote mbili kuachana na tofauti zao na kukubali mpango utakaotoa muongozo wa majadiliano ya amani na kusema kuwa kutahitajika muda zaidi na kujitolea.

Maafisa wa Marekani wamekana kusema kilicho ndani ya mapendekezo ya Kerry lakini wakasema wanatumai kukamilisha hivi karibuni.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP

Mhariri: Sekione Kitojo