Kerry aitaka Syria kuruhusu uchunguzi
25 Agosti 2013Wakaguzi wa silaha wa Umoja wa Mataifa wanatakiwa kuingia katika maeneo yanayodaiwa kuwa shambulio la gesi ya sumu limefanyika.
Kerry amepiga simu "kuweka wazi kuwa iwapo , kama inavyodaiwa, serikali ya Syria haina cha kuficha, inapaswa kuwaruhusu wakaguzi mara moja na wapewe ruhusa bila ya vipingamizi katika maeneo hayo badala ya kuendelea kuyashambulia maeneo yaliyoathirika na kuzuwia kuingia kwa wakaguzi pamoja na kuharibu ushahidi" wizara ya mambo ya kigeni imesema.
Uhakikisho
"Waziri Kerry amesisitiza zaidi kwamba amepokea uhakikisho kamili kutoka kwa makamanda wa jeshi la Syria kuwa watahakikisha kuingia kwa salama wakaguzi wa umoja wa Mataifa katika maeneo hayo," amesema afisa wa wizara hiyo.
Kerry ambaye alishiriki akiwa hayupo katika Ikulu ya Marekani ya White House katika mkutano kuhusiana na uwezekano wa Marekani kuchukua hatua dhidi ya kile kinachodaiwa kuwa ni matumizi ya silaha za kemikali nchini Syria, amefanya mawasiliano kadha na wanadiplomasia kadha jana Jumamosi na mawaziri wenzake nchini Saudi Arabia , Jordan na Uturuki, afisa huyo amesema.
Katika mazungumzo yote hayo kwa njia ya simu , waziri Kerry amesisitiza umuhimu wa utambuzi wa haraka wa ukweli na kueleza umihumu na athari za matumizi ya silaha za kemikali, ameongeza afisa huyo.
Marekani na Uingereza zajadiliana
Rais wa Marekani pamoja na waziri mkuu wa Uingereza David Cameron wamekaribia jana Jumamosi kuweka lawama za shambulio hilo la gesi ya sumu karibu na mji mkuu Damascus mikononi mwa majeshi ya rais Bashar al-Assad.
Taarifa kutoka ofisi ya waziri mkuu katika mtaa wa Downing imesema kuwa viongozi wa Marekani na Uingereza , wana wasi wasi mkubwa , kuhusiana na ishara zinazoongezeka kuwa hilo lilikuwa shambulio la silaha za kemikali lililofanywa na utawala wa Syria dhidi ya watu wake.
"Ukweli kwamba rais Assad ameshindwa kutoa ushirikiano na Umoja wa Mataifa kunaashiria kuwa utawala huo una kitu cha kuficha," taarifa hiyo imeongeza, na kudokeza kuwa " matumizi ya silaha la kemikali yatasababisha kuchukuliwa hatua kali kutoka jumuiya ya kimataifa."
Serikali ya Syria pamoja na mahasimu wake wakati huo huo wametupiana lawama kwa matumizi hayo ya silaha za sumu, wakati shirika la kutoa misaada la madaktari wasio na mipaka limesema kiasi ya watu 355 wamefariki kutokana na dalili za "sumu inayoathiri mapafu" kutokana na shambulio la Jumatano, huku maelfu zaidi wakipatiwa matibabu hospitalini.
Iwapo itathibitishwa , shambulio hilo litakuwa baya kabisa la matumizi ya gesi ya sumu tangu Saddam Hussein kutumia gesi ya sumu dhidi ya wanajeshi wa Iran na maeneo ya waasi wa Kikurdi kaskazini mwa Iraq katika miaka ya 1980.
Huenda mambo yameiva
Mazungumzo ya Obama na washauri wake wa masuala ya usalama yamekuja siku moja baada ya waziri wa ulinzi Chuck Hagel kusema wizara yake imewasilisha mapendekezo kadha kwa rais na ameeleza kuwa majeshi ya Marekani yanasogezwa karibu kwa uwezekano wowote wa uamuzi wa kuchukua hatua dhidi ya utawala wa Syria.
Wakati huo huo mkuu wa idara ya kupunguza silaha duniani wa Umoja wa Mataifa , Angela Kane, amewasili mjini Damascus siku ya Jumamosi ( 24.08.2013) kutoa msukumo kwa serikali ya Syria kuwaruhusu wataalamu wa Umoja huo kuchunguza madai ya matumizi ya silaha za sumu.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri : Amina Aboubakar