Kerry amshtumu Assad kukwamisha mazungumzo
17 Februari 2014Waziri Kerry amesema baada ya kufanya mazungumzo na mwenzake wa Indonesia Marty Natalegawa mjini Jakarta, kwamba utawala wa rais Assad umekwamisha mazungumzo hayo, na haujafanya chochote zaidi ya kuendelea kuangusha mabomu ya mapipa dhidi ya raia wake. Kerry amesema ni wazi kwamba Bashar al-Assad anaendelea kujaribu kushinda katika uwanja wa vita kuliko kuja katika meza ya mazungumzo kwa nia njema.
Waziri huyo wa mambo ya kigeni wa Marekani alisema upinzani uliwasilisha mpango uliyotafakariwa sana na wenye hoja nzuri, wa kuanzisha chombo cha uongozi wa mpito. Duru ya hivi karibuni ya mazungumzo ya nchini Uswisi ilishindwa kufuatia kukataa kwa serikali ya rais Bashar al-Assad kutilia maanani uundwaji wa serikali ya mpito, ambamo upinzani ungeshiriki.
Brahimi azitaka pande zitafakari
Mpatanishi wa kimataifa Lakhdar Brahimi alisema mjini Geneva siku ya Jumamosi, kwamba duru mbili za kwanza za mazungumzo hayo hazijapiga hatua yoyote muhimu, lakini kwamba pande mbili zilikubaliana juu ya ajenda ya duru ya tatu katika tarehe ambayo haikutajwa.
"Kwa hivyo nadhani ni bora kila upande urudi utafakari na uchukuwe wajibu wake. Wanataka mchakato huu unendelee au la? Na mimi nitafanya hivyo. Nitarudi na kuzungumza na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon," alisema Brahimi.
Upinzani unasema fokasi ya mazungumzo laazima iwe juu ya kuundwa kwa serikali ya mpito bila Assad. Lakini wawakilishi wa utawala wamesisitiza kuwa nafasi ya Assad haina mjadala, na wamekataa kujadili jambo lolote zaidi ya ugaidi, ambao serikali inaulamu kwa wapinzani wake na wafadhili wao wa magharibi.
Brahimi alisema kuwa pande mbili zitakaporudi, watajadili kwanza juu ya machafuko na ugaidi na badaye uundaji wa chombo cha uogozi wa mpito, hayo yakifuatiwa na mjadala juu ya taasisi za kitaifa, na mwishowe maridhiano ya kitaifa na mjadala wa kitaifa.
Lakini raia wa Syria wanaonekana kukatishwa tamaa na mazungumzo hayo. "Tulikuwa tuna matumaini ya kurudi nyumbani, lakini matumaini hayo yote yamepotea. Geneva 1, Geneva 2, Geneva 3 au 4 au 5, hakuna kitakachosaidia, na badala yake mgogoro unazidi kuwa mbaya, na muda wa utawala unazidi kuwa mrefu," alisema Abu Ahmed, ambaye ni mkimbizi wa Syria.
Urusi yatiwa kishindo
Waziri Kerry pia ameitaka Urusi kuacha kuuzia utawala huo silaha, akiiambia Moscow kuwa inahitaji kuwa sehemu ya suluhisho. Alisema wakati mazungumzo hayo yako katika kipindi cha mapumziko, dunia inapaswa kufahamu kuwa hakuna mapumziko kwa watu wa Syria wanaoendelea kuteseka.
Urusi inasema mazungumzo hayo hayapaswi kujikita tu katika kuunda serikali ya mpito, na imezishtumu serikali za magharibu kwa kushinikiza mabadiliko ya utawala.
Rais wa Marekani Barack Obama alisema Ijumaa wiki iliyopita kuwa alikuwa anatafakari njia nyingine za kumshinikiza Assad, lakini hakutoa maelezo zaidi.
Shirika la haki za binaadamu la Syria lenye makao yake jijini London Uingereza, lilisema wiki iliyopita kuwa idadi ya vifo vilivyotokana na vita hivyo vilivyoanza mwaka 2011, imevuka 140,000
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe, rtre, dpae
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman