1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kerry ashinikiza amani Mashariki ya Kati

3 Januari 2014

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry Ijumaa(03.01.2014) ameingia siku ya pili ya mazungumzo na Wapalestina na Waisrael kuanzisha msingi wa mchakato utakawaongoza kwenye njia ya kufikia makubaliano ya amani.

https://p.dw.com/p/1Akkd
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu katika mkutano na waandishi wa habari mjini Jerusalem. (02.01.2014).
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu katika mkutano na waandishi wa habari mjini Jerusalem. (02.01.2014).Picha: Brendan Smialowski/AFP/Getty Images

Maafisa wa Marekani wamesema faraghani kwamba wanaamini mazungumzo hayo ya ana kwa ana yalioanza upya mwezi wa Julai baada ya kukwama kwa miezi mitatu yamefikia awamu mpya wakati muda wa mwisho uliowekwa kufikia kwa makubaliano hapo mwezi wa Aprili ukikaribia lakini wamesema wako mbioni kuondokana na upinzani mkali kutoka pande zote mbili dhidi ya kufikia muafaka wa aina yoyote ile.

Kerry hapo jana amerudi tena Israel kwa ziara yake ya 10 akiwa kama waziri wa mambo ya nje wa Marekani na moja kwa moja alikwenda kuonana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu katika mikutano iliochukuwa saa tano.

Wanataraji kukutana tena leo mchana baada ya Kerry na timu yake kukutana na waziri wa mambo ya nje wa Israel Avigdor Lieberman mjini Jerusalem hapo asubuhi.

Baadae Kerry ataelekea Ramallah kwa mazungumzo na Rais wa Mamlaka ya Wapalestina Mahmud Abbas katika makao yake ya Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Israel.

Netanyahu amshutumu Abbas

Lakini Netanyahu hapo jana hakuyawekea matumaini makubwa mazungumzo hayo na kumshambulia vikali Rais Abbas kwa kuelezea wasi wasi wake iwapo yeye na Wapalestina wana nia ya dhati katika shauku yao ya kuwa na amani.

Rais Mahmud Abbas wa Mamlaka ya Wapalestina akizungumza mjini Ramallah wakati wa kuwakaribisha wafungwa 26 walioachiiwa na Israel.(31.12.2013).
Rais Mahmud Abbas wa Mamlaka ya Wapalestina akizungumza mjini Ramallah wakati wa kuwakaribisha wafungwa 26 walioachiiwa na Israel.(31.12.2013).Picha: Reuters

Netanyahu alimwambia Kerry na hapa nanukuu." Nafahamu umejizatiti kwa amani, nafahamu kwamba mimi mwenyewe nimejitolea kwa ajili amani.Lakini kwa bahati mbaya kwa kuzingatia vitendo na maneno ya viongozi wa Wapalestina, kuna wasi wasi unaozidi kuongezeka nchini Israel iwapo kweli Wapalestina wamejitolea kwa amani." mwisho wa kunukuu.

Alikuwa akukusudia juu ya kuachiliwa kwa wafungwa wa Kipalestina waliokuwa wakishikiliwa kwa muda mrefu katika magereza ya Israel kama sehemu ya mazungumzo hayo,ambapo kiongozi huyo wa Israel amesema Abbas amewapokea na kuwakumbatia magaidi hao kama ni mashujaa.Amesema kuwatukuza wauaji wa wanawake na wanaume wasiokuwa na hatia kuwa ni mashujaa ni jambo la kukirihisha.

Amesema hawezi kuwa dhidi ya magaidi wakati huo huo akiwaunga mkono magaidi.

Marekani yajizatiti kwa amani

Lakini Kerry ameapa kwamba Marekani imejizatiti kushirikiana na pande zote mbili kupunguza tafauti zao katika kuwa na mchakato wa msingi ambao utatowa miongozo ya kuwa na mazungumzo ya kufikia makubaliano ya mwisho.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mjini Jerusalem.(02.01.2014).
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mjini Jerusalem.(02.01.2014).Picha: Brendan Smialowski/AFP/Getty Images

Machakato huo utaainisha makubaliano na kile wasichokubaliana katika masuala ya msingi yenye kuzigawanisha pande hizo mbili ikiwa ni pamoja na ramani ya taifa la baadae la Palestina,wakimbizi,hatima ya Jerusalem,usalama, kila taifa kulitambuwa taifa la mwenzake na kukomesha mzozo pamoja na madai mengine yote.

Kerry amesema kutokana na mchakato huo pande zote zitajuwa kule zinakoelekea na matokeo ya mwisho yatakuwaje.

Wapalestina wanataka mipaka yao iwe ile iliokuweko mwaka 1967 kabla ya Vita vya Siku Sita wakati Israel ilipouteka Ukanda wa Magharibi ikiwa ni pamoja Jerusalem ya mashariki inayokaliwa na Waarabu ambayo hivi sasa wameitwaa kwa nguvu.

Lakini Israel inataka kuendelea kushikilia maakazi ya walowezi wa Kiyahudi iliyoyajenga ndani ya ardhi ya Wapalestina iliokuwa imeikalia kwa mabavu tokea wakati huo.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman