Kesi katika mauaji ya Khashoggi yaanza
3 Januari 2019Mahakama ya kifalme imesema hayo wakati ikifanya kikao chake cha kwanza kusikiliza kesi hiyo.
Saudi Arabia imesema pia imetuma barua kwa mwendesha mashitaka wa serikali ya Uturuki ikiomba "ushahidi wowote unaohusiana na kesi hiyo", ambayo imeutikisa uongozi wa kifalme nchini Saudi Arabia na kuchafua heba ya mwanamfalme mteule Mohamed bin Salman mwenye umri wa miaka 33.
Khashoggi alikuwa karibu na duru za jumba la ufalme wa Saudia kabla ya kuwa mkosoaji mkubwa wa mwanamfalme Mohammed na kuanza kuandika katika jarida la Washington Post na kuzungumza katika vyombo vya habari vya kimataifa juu ya siasa za Saudia na hatimaye kuhamia nchini Marekani mwaka jana.
Maafisa wa Saudia wamekataa shutuma kwamba mwanamfalme mteule aliamuru kuuwawa katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul, ambamo mwili wa Khashoggi ulikatwakatwa, kuondolewa kutoka katika jengo hilo na kukabidhiwa kwa " mtu aliyeshirikishwa nchini humo" ambaye hajajulikana.
Yaliko mabaki ya mwili wa Khashoggi bado hakujulikani, lakini televisheni moja ya Uturuki siku ya Jumatatu ilionesha watu wakibeba masanduku ambayo huenda yalikuwa na mabaki ya mwili wa Khashoggi na kuingiza katika makaazi ya balozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul.
"Kesi hiyo inayowahusu watu 11 inayoanza kusikilizwa kwa mara ya kwanza na mwendesha mashitaka wa serikali katika kesi ya mauaji ya raia Jamal Khashoggi ilifanyika leo, katika mahakama ya uhalifu ya kifalme mjini Riyadh," taarifa kutoka katika ofisi ya mwendesha mashitaka wa Saudia iliyochapishwa na shirika la habari la SPA ilisema.
Ofisi ya mwendesha mashitaka imesema inataka hukumu ya kifo kwa watu watano kati ya 11 walioshitakiwa.
Watuhumiwa wengine 10 bado wako chini ya uchunguzi. Shirika la habari la SPA limeongeza kwamba wakili wa washitakiwa amehudhuria kikao hicho na mahakama iliidhinisha ombi la watu hao 11 ambao wameomba kupatiwa muda zaidi kuweza kutayarisha utetezi wao. Shirika hilo la habari hata hivyo halikutoa maelezo zaidi kuhusiana na kikao kijacho.
Taarifa hiyo imesema kuwa nchi hiyo ya kifalme inasubiri jibu la maombi juu ya taarifa iliyotumwa kwa maafisa wa Uturuki.
Mwaka uliopita, Mfalme wa Saudia Salman alimteua Ibrahim al-Assaf , waziri wa zamani wa fedha , katika wadhifa wa waziri wa mambo ya kigeni, katika juhudi za kuimarisha taswira ya ufalme huo baada ya mzozo huo uliosababishwa na mauaji hayo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Grace Patricia Kabogo