1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya George Floyd: Maafisa wengine watatu washitakiwa

Daniel Gakuba
4 Juni 2020

Mwendeshamashtaka mkuu wa jimbo la Minnesota nchini Marekani ameongeza uzito wa mashtaka dhidi ya afisa wa polisi mweupe aliyemkaba koo kwa goti lake George Floyd, Mmarekani mweusi aliyekufa akiwa mikononi mwa polisi.

https://p.dw.com/p/3dEob
USA Minneapolis Polizei |Tod eines Schwarzen Mannes
Picha: AFP/Facebook/Darnella Frazier

Mashtaka dhidi ya mtuhumiwa mkuu katika kifo hicho cha George Floyd, aliyekuwa afisa wa polisi Derek Chauvin yamepandishwa kutoka mauaji ya daraja la tatu ambayo sio ya kukusudia, hadi daraja la pili, ambalo linahusisha dhamira ya kuuwa, au mauaji yaliyosababishwa na uzembe na kutojali. Adhabu ya mauaji ya aina hiyo nchini Marekani inaweza kufika miaka 40 jela.

Maafisa wengine watatu waliokuwa pamoja na Derek Chauvin pia wamekamatwa na kufunguliwa mashtaka. Wawili miongoni mwao walionekana kumkanyaga mgongoni marehemu Floyd wakati Chauvin alipokuwa amemkaba koo, na mwingine alisimama kando akitazama tu bila kufanya chochote.

Kumpata na hatia polisi wa Marekani ni kazi ngumu

USA Washington DC | Proteste gegen Polizeigewalt vor dem weißen Haus
Maandamano makubwa yameshuhudiwa kote Marekani na kwingineko kupinga ukatili wa polisi hususan dhidi ya Wamarekani weusiPicha: imago images/UPI Photo/T. Katopodis

Mwendeshamashtaka mkuu wa jimbo la Minnesota Keith Ellison almesema kumtia hatiani afisa wa polisi nchini Marekani ni mchakato mgumu sana, ambao unachukua muda mrefu, na kusikitika kuwa hali hiyo imeharibu imani ya umma kwa mfumo wa sheria.

''Nitakuwa mkweli hapa, kesi za aina hii hazikupewa uzito jimboni Minnesota na nchini kote Marekani, na nadhani kuporomoka kwa imani kumetokana na historia ndefu ya kukosa utashi wa kuwawajibisha wale wenye majukumu ya kusimamia uwajibikaji katika jamii'' amesema mwendeshamashtaka mkuu huyo, na kuongeza kuwa ingawa hawawezi kudhibiti yaliyopita, ''tunao wajibu wa kushughulikia vyema kesi hii na kuhakisha haki inatendeka, na tutafanya hivyo.''

Kifo cha George Floyd na mazingira yake viligusa hisia za watu kote ulimwenguni, na kuzusha maandamano ambayo wakati mwingine yamekumbwa na ghasia na uporaji. Watu 12 wamepoteza maisha katika maandamano hayo, lakini bado hakuna maelezo ya kutosha kuhusu walivyokutwa na mauti. Vyombo vya usalama vimewatia mbaroni watu wapatao 10,000 kote Marekani kuhusiana na ghasia hizo.

James Mattis
Waziri wa zamani wa ulinzi Jim Mattis amesema Trump anajaribu kuwagawanya wananchi wa MarekaniPicha: picture-alliance/AP Photo/S. Walsh

Rais Trump azidi kukosolewa

Wakati huo huo ukosoaji umeendelea dhidi ya namna Rais wa nchi hiyo Donald Trump anavyoushughulia mzozo huo. Wa hivi karibuni kupaza sauti yake ni aliyekuwa waziri wake wa ulinzi Jim Mattis, ambaye amemtuhumu rais huyo kuwa na nia ya kuwagawa wananchi wa Marekani, na ameshindwa kutoa uongozi unaohitajika wakati wa mgogoro.

Hapo jana, waziri wa sasa wa ulinzi Mark Asper, alipinga pendekezo la Rais Trump, kutaka wanajeshi wapelekwe mitaani kuzima ghasia na maandamano, akisema hali haijafika katika kiwango hicho.

Naye Rais wa zamani Barack Obama ameunga mkono vuguvugu la maandamano baada ya kifo cha George Floyd, na kuelezea matumaini yake kuwa yanaweza kuwa mwanzo wa mabadiliko.

 

dpae, ape