Kesi ya kumshtaki Trump yaanza Baraza la Seneti
17 Januari 2020Kesi hiyo ilianza huku maseneta wakisimama na kula kiapo cha kusimamia haki bila upendeleo kama majaji, waendesha mashtaka wa baraza hilo wakisoma mashtaka, na mwanasheria mkuu John Roberts akiongoza kesi hiyo.
Maseneta wanne wanaosimamia kesi hiyo, wanachuana ili mmoja wao kuteuliwa kama mgombea urais kupitia tiketi ya chama cha Democtratic na kupambana na Trump katika uchaguzi ujao.
Trump anakabiliwa na mashtaka mawili baada ya Baraza la Wawakilishi kupiga kura ya kumshtaki mwezi uliopita, moja likiwa ni matumizi mabaya ya madaraka yake kwa kuishinikiza Ukraine kumchunguza hasimu wake wa chama cha Democratic Joe Biden. Trump pia anashtakiwa kuzuia uchunguzi dhidi yake uliofunguliwa baadae na Bunge.
Rais huyo anaendelea kusisitiza kuwa hana makosa. Na Alhamisi kwa mara nyingine tena ameyatupilia mbali mashtaka hayo na kusema kuwa ni uwongo mtupu.
Soma zaidi:Baraza la Seneti kusikiliza shauri dhidi ya Trump
Trump hatarajiwi kukutikana na hatia katika baraza hilo linalohodhiwa na maseneta wa chama chake cha Republican. Hata hivyo kuna ushahidi mpya unaodhihirisha vitendo vya Trump dhidi ya Ukraine.
Ushahidi mpya wazua mjadala
Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi imesema Alhamisi kwamba serikali ya Trump ilikiuka sheria ya nchi kwa kuzuia msaada wa usalama kwa Ukraine, ambayo ina mpaka mmoja na Urusi yenye uadui nayo.
Wakati huo huo, mshirika wa wakili binafsi wa Trump Rudy Giuliani, Lev Parnas, ambaye naye ameshtakiwa amewasilisha nyaraka za ushahidi mpya kwa waendesha mashtaka unaomhusisha rais huyo na sera ya kigeni isiyo rasmi inayoendeshwa na Giuliani. Ushahidi huo mpya umewashinikiza maseneta kuita mashahidi wapya katika kesi hiyo, hali iliyozua mabishamo ambayo bado hayakupatiwa suluhisho.
Spika wa Bunge Nancy Pelosi alisema ushahidi huo mpya kutoka kwa Parnas unahitaji kufanyiwa uchunguzi, ambao hautarajii kufanywa na Mwanasheria Mkuu wa Trump.
Baraza hilo la Seneti litatoa wito rasmi kwa Ikulu ya Rais kuhudhuria katika kikao hicho, na timu ya kisheria ya rais inatarajiwa kutoa jibu Jumamosi. Hoja za mawakili zitaanza kusikilizwa Jumanne.
Wiki ijayo, wakati Baraza la Seneti likisikiliza hoja za ufunguzi wa kesi hiyo, Trump atakuwa katika mji wa mapumziko wa Davos nchini Uswisi mbali na mvutano huo kati ya vyama vya Democratic na Republican.
Vyanzo: (ap,afp)