Kesi ya Ratko Mladic yafunguliwa The Hague
16 Mei 2012Mladic anashitakiwa kwa kuongoza mauaji ya kikatili ya Waislamu 8,000 wengi wao vijana na watu wazima huko Srebrenica mnamo mwaka wa 1995. Hayo ndiyo mauaji ya kikatili zaidi tangu kumalizika kwa vita vya pili vya dunia.
Ratco Mladic ambaye sasa ana umri wa miaka 70, ndiye mhusika wa mwisho katika vita vya eneo la Balkan katika miaka ya tisini kufunguliwa mashitaka katika mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kwa iliyokuwa Yugoslavia mjini The Hague.
Anatuhumiwa kwa kuchochea siyo tu wiki nzima ya mauaji ya kikatili mjini Srebrenica, bali pia kuzingirwa Sarajevo kwa miezi 43 ambapo zaidi ya watu 10,000 waliuwawa na walenga shabaha, na makombora.
Mashitaka 11
Orodha ya mashitaka 11 yanayomkabili Mladic kama Kamanda wa jeshi la Serbia katika vita vya Bosnia vya mwaka wa 1992 – 95 ni pamoja na mauaji ya halaiki, vitendo vya kigaidi, na uhalifu mwingine dhidi ya binadamu.
Mladic alikamatwa mwezi Mei mwaka jana baada ya miaka 16 ya kuwa mafichoni, amekanusha mashitaka hayo akisema ni ya kuchusha mno akiongeza kuwa yeye ni mgonjwa sana hivyo hawezi kuendelea na kesi. Mahakama hiyo ilitoa tamko kwa niaba yake kwamba hana hatia.
Akiwa amevalia suti ya kijivu na tai nyeusi, Mladic aliwaamkua majaji na kuwashangilia wafuasi wake wakati akiingia mahakamani wakati kesi yake ikianza leo. Kila mara alionekana akiandika maelezo na hakuonyesha hisia zozote wakati waendesha mashitaka walianza kufafanua uhalifu anaodaiwa kufanya.
Jaji Kiongozi Alphons Orie wa Uholanzi alisema awali ya yote mahakama hiyo inatathmini kuhairisha kuwasilisha ushahidi, ambao untarajiwa kuanza tarehe 29 Mei, kutokana makosa kwa upande wa waendesha mashitaka katika kufichua ushahidi kwa upande wa mshtakiwa. Mwendesha mashitaka Demort Groome alisema hatapinga hatua yoyote ya kuhairisha ushahidi.
Uhalifu ulipangwa
Groome alifungua taarifa yake kwa kumwangazia mvulana mwenye umri wa miaka 14 ambaye babake na mjombake walikuwa miongoni mwa wanaume 150 waliouwawa na wanajeshi wa Waserbia wa Bosnia mwezi Novemba mwaka 1992. alisema mauaji yote yaliyofanywa mjini Srebrenica Mladic yalipangwa.
Kisha akawaonyesha majaji mkanda wa video wa mauaji yaliyofanywa katika soko la Markale katika mji mkuu wa Bosnia, Sarajevo, ambapo watu kadhaa waliuwawa.
Alisema mashambulizi hayo yalikuwa mpango wa kuwaangamiza raia wasio wa Serbia katika ardhi ya Bosnia. Groome amesema waendesha mashitaka wataonyesha ushahidi kubainisha kuwa Mladic alichangia katika kila ya aina ya uhalifu huo. Jenerali huyo alikataa kutoa tamko mbele ya mahakama kuhusu mashitka hayo lakini anakanusha kufanya makosa yoyote, akisema kuwa alifanya hivyo kuwalinda Waserbia ndani ya Bosnia. Ikiwa atapatikana na hatia, Mladic anaweza kupewa kifungo cha juu cha maisha gerezani.
Kiongozi wa zamani wa kisiasa wa Waserbia wa Bosnia Radovan Karadzic tayari anaendelea na kesi yake katika mahakama hiyo.
Mwandishi: Bruce Amani/APE
Mhariri: Abdu Mtullya