1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kevin-Prince Boateng arudi katika Bundesliga

Josephat Nyiro Charo31 Agosti 2013

Kiungo wa AC Milan, Kevin-Prince Boateng, amejiunga na Schalke 04 kwa mkataba wa miaka mitatu siku ya Ijumaa (30.08.2013). Anakiri ana furaha kurejea katika ligi ya Ujerumani, Bundesliga.

https://p.dw.com/p/19ZMd
FC Schalke 04 Neuzugang Kevin-Prince Boateng hält am 30.08.2013 in Gelsenkirchen (Nordrhein-Westfalen) neben Schalkes Trainer Jens Keller (l) und Manager Horst Heldt (r) bei seiner Präsentation auf einer Pressekonferenz des Fußball-Bundesligisten ein Trikot hoch. Foto: Caroline Seidel/dpa
Deutschland Fußball FC Schalke 04 Neuzugang Kevin-Prince BoatengPicha: picture-alliance/dpa

Inaripotiwa kwamba Schalke iliwalipa wataliana euro milioni 12 kumpata Kevin -Prince Boateng, nyota wa timu ya taifa ya kandanda ya Ghana. na mkataba wake unajumuisha uwezekano wa kuongezewa msimu wa nne. "Bundesliga ndio ligi nzuri kabisa ulimwengu na ndiko wachezaji bora duniani wanakokwenda," alisema mchezaji huyo wa umri wa miaka 26 katika mkutano na waandishi wa habari mjini Gelsenkirchen. "Nimesema kila mara kwamba nilitaka kucheza nchini Ujerumani."

Kevin, ambaye ni kakake mchezaji wa safu ya ulinzi wa timu ya Bayern Munich na timu ya taifa ya Ujerumani, Jerome Boateng, alianza kibarua cha kucheza soka katika klabu ya Hertha Berlin na kuhamia Tottenham Hotspur, England, kwa kitita cha euro milioni 7.9 mnamo mwaka 2007. Alirejea kwa muda mfupi Ujerumani kwa mkopo katika timu ya Borussia Dortmund, mahasimu wa Schalke, kabla kujiunga na Portsmouth na baadaye kwenda Milan.

Ni mchezaji mahiri

Boateng alifunga mabao mawili katika ushindi wa Milan siku ya Jumatano dhidi ya PSV Eindhoven katika duru ya pili ya mchuano wa mchujo na kufaulu kushiriki mashindano ya kuwania kombe la mabingwa wa Ulaya, Champions League, msimu huu kwa jumla ya magoli 4-1.

epa03840864 AC Milan's Ghanaian midfielder Kevin-Prince Boateng (R) celebrates with his teammate Mattia De Sciglio (L) after scoring the opening goal during the UEFA Champions League playoff second leg soccer match between AC Milan and PSV Eindhoven at Giuseppe Meazza stadium in Milan, Italy, 28 August 2013. EPA/MATTEO BAZZI +++(c) dpa - Bildfunk+++
Kevin wakati wa mechi kati ya Milan na PSV EindhovenPicha: picture-alliance/dpa

"Ni mchezaji wa kipekee mwenye uwezo mkubwa na ujuzi wa uongozi," amesema kocha wa Schalke, Jens Keller. Pamoja na nyota wa Schalke, Julian Draxler, mwenye umri wa miaka 19, Boateng huenda akaunda ushirikiano imara. Meneja wa Schalke, Horst Heldt, amefutilia mbali uwezekano wa kumuuza Draxler kabla muda wa wachezaji kuhamia timu nyengine kumalizika wiki ijayo. "Itakuwa hatua ya kuchanganyikiwa kumpa mkataba mchezaji mzuri kisha baadaye umuache mwingine aondoke. Hilo silo tunalolitaka," akaongeza kusema Heldt.

Boateng anaweza kucheza katika mechi ya leo dhidi ya Leverkusen, licha ya kufungiwa mechi nne wakati alipotolewa uwanjani kwa kumpiga usoni mchezaji wa timu nyingine katika mechi yake ya mwisho kati ya Dortmund na Wolfsburg mnamo mwaka 2009.

Mwandishi: Josephat Charo

Mhariri: Caro Robi