1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa Juu Iran aapa kulipiza kisasi dhidi ya Israel

Hawa Bihoga
3 Novemba 2024

Kiongozi wa juu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, ameapa kulipiza kisasi dhidi ya Israel kufuatia mashambulizi ya hivi karibuni yaliosababisha hasara kubwa.

https://p.dw.com/p/4mXfl
Iran | Ayatollah Ali Khamenei
Kiongozi wa juu wa Iran, Ayatollah Ali KhameneiPicha: Iranian Leader Press Office/Anadolu/picture alliance

Kauli hiyo ameitoa wakati maafisa nchini Iran wanazidi kutishia kuishambulia tena Israel, baada ya mashambulizi yake ya Oktoba 26 dhidi ya vituo vya kijeshi na maeneo mengine ya Iran, yalioua watu wasiopungua watano. 

Akizungumza siku chache kabla ya uchaguzi wa Marekani, Kiongozi huyo wa Juu wa Iran ameonya kuwa Marekani na Israel zitakabiliwa na matokeo makubwa kwa vitendo vyao. 

"Vitendo vya adui havitasahaulika kwa wale wanaowakilisha taifa la Iran. Havitasahaulika. Maadui - ambao ni Marekani au utawala wa Kizayuni, wanapaswa kujua kwamba watapata majibu makali kwa kile wanachofanya dhidi ya Iran, taifa la Iran, na safu ya upinzani."

Soma pia:Israel katika hali ya tahadhari kufuatia kitisho cha Iran

Marekani imeionya Iran katika siku za karibuni dhidi ya kuishambulia tena Israel, huku maafisa wake wakisema kuwa Washington haitaweza kuizuwia Israel ikiwa itashambulia tena.

Gazeti la Axios limeripoti kuwa taarifa za ujasusi za Israel zinaonyesha Iran inajiandaa kuishambulia Israel kwa kutumia ardhi ya Iraq katika siku zijazo, yumkini kabla ya uchaguzi wa Marekani kesho kutwa.

Wakati huo huo, ndege za kivita za Marekani za B-52 zimepelekwa Mashariki ya Kati kama onyo kwa Tehran.