KHARTOUM: Annan atembelea kambi ya wakimbizi katika jimbo la Darfur
28 Mei 2005
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,Kofi Annan amelizuru eneo la mgogoro la Darfur,hiyo ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku 3 nchini Sudan.Baada ya kuwa na majadiliano pamoja na waziri wa kigeni wa Sudan Mustafa Osman Ismael,mjini Khartoum,Annan alielekea Nyala,mji mkuu wa jimbo la Darfur.Huko aliizuru kambi ya Kalma ambayo ni kambi kubwa kabisa ya wakimbizi duniani.Tangu miaka miwili iliyopita,kiasi ya watu 110,000 huishi katika kambi hiyo.Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya watu 180,000 wameuawa na wengine wapatao milioni 2.4 wamelazimika kuhama makwao kwa sababu ya mapigano.Tangu Februari mwaka 2003,wanamgambo wenye asili ya Kiarabu walio karibu na serikali ya Khartoum wamekuwa wakiwashambulia wakazi wa Darfur.Katibu Mkuu Kofi Annan,anataka kuyafufua majadiliano ya amani yaliovunjika tangu mwezi wa Desemba.