1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KHARTOUM : Umoja wa Afrika wayakinisha kuondoka Dafur

5 Septemba 2006
https://p.dw.com/p/CDFE

Sudan imesema hapo jana itaruhusu vikosi vya Umoja wa Afrika kubakia huko Dafur ikiwa tu vitakuwa chini ya udhibiti wa Umoja wa Afrika na imeshutumu serikali ya Marekani kwa kujaribu kuleta mabadiliko ya serikali nchini Sudan kwa kutaka kupeleka jeshi la Umoja wa Mataifa.

Sudan ilizusha hofu ya kuzuka kwa vita kamili katika jimbo lake la vurugu la Dafur kwa kusema hapo Jumapili kwamba vikosi vya Umoja wa Afrika lazima viondoke wakati muda wa mamlaka ya kuwepo kwao huo Dafur utakapomalizika.

Umoja wa Afrika uliyakinisha kwamba wanajeshi wake wa kulinda amani wataondoka kwenye jimbo hilo la Dafur nchini Sudan mwishoni mwa mwezi wa Septemba.

Umoja wa Afrika umesema unataka kikosi cha Umoja wa Mataifa kuchukuwa nafasi yake hatua ambayo inapingwa vikali na serikali ya Sudan.

Rais Omar al Bashir wa Sudan amekiita kikosi hicho cha Umoja wa Mataifa kuwa sehemu ya mpango wa kutaifisha haki ya kujitawala ya nchi hiyo.

Alhamisi iliopita Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la kuweka zaidi ya wanajeshi 20,000 wa kulinda amani kuchukuwa nafasi ya kikosi cha wanajeshi 7,000 wa Umoja wa Afrika kinachokabiliwa na uhaba wa fedha za kukihudumia .

Vita na Njaa vimesababisha watu 300,000 kupoteza maisha yao na kuwapotezea makaazi wengine milioni mbili na nusu huko Dafur.