1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Khartoum. Walinzi wa amani wa jeshi la umoja wa Afrika watekwa.

10 Oktoba 2005
https://p.dw.com/p/CETO

Kundi la waasi limewakamata mateka kiasi cha wanajeshi 40 wa jeshi la kulinda amani la umoja wa Afrika jana Jumapili katika jimbo lenye machafuko la Dafur, magharibi ya Sudan , siku moja baada ya wanajeshi watatu pamoja na wakandarasi wawili kuuwawa.

Msemaji wa umoja wa Afrika AU Nourredine Mezni ameliambia shirika la habari la AFP kuwa baadhi ya mateka wameachiliwa huru siku hiyo hiyo , lakini hakuweza kutoa idadi ya walioachiwa.

Msemaji huyo amesema kuwa kwa mujibu wa taarifa alizonazo, watu hao walioachiwa wanatembea hivi sasa kwa miguu kwenda katika kituo cha umoja wa Afrika katika jimbo la Tina, na kuongeza kuwa ni pale tu watu hao watakapowasili ndipo kutakuwa na uwezekano wa kueleza idadi kamili ya watu walioachiwa.

Umoja wa Afrika umelilaumu kundi la Sudan Liberation Army, SLA, tawi la kijeshi la waasi wa Sudan Liberation Movement SLM, kwa mapambano yaliyotokea siku ya Jumamosi karibu na Menawasha katika njia ya Khor Abeche kusini mwa jimbo la Darfur.