1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KHARTOUM : Wanajeshi wawili wa Umoja wa Afrika wauwawa

20 Agosti 2006
https://p.dw.com/p/CDK8

Wanajeshi wawili wa Umoja wa Afrika wameuwawa na wengine watatu kujeruhiwa katika shambulio kwa mojawapo ya misafara yao katika jimbo la Dafur nchini Sudan hapo jana.

Taarifa ya Umoja wa Afrika imesema Kikosi cha Umoja wa Afrika AMIS kinalaani kwa nguvu zote shambulio hilo ovu dhidi ya wanajeshi wake huko Dafur na inakusudia kufanya uchunguzi kikamilifu.

Shambulio hilo lililenga msafara uliokuwa umebeba mafuta katika eneo la Kouma kama kilomita 80 kaskazini mashariki ya mji mkubwa wa Dafur wa el-Fasher.Eneo hilo liko chini ya udhibiti wa waasi ambao hakuwasaini makubaliano ya amani ya mwezi wa Mei lakini Umoja wa Afrika umesema bado haifahamiki bayana ni nani waliohusika wa shambulio hilo.

Duru za Umoja wa Afrika zimesema wanajeshi hao walioshambuliwa walikuwa wanatoka Rwanda.

Kuna wanajeshi 7,000 wa Umoja wa Afrika wanaolinda amani huko Dafur na Nigeria,Senegal na Afrika Kusini ndio nchi zenye wanajeshi wengi katika kikosi hicho.