Kifo cha mwisho kabla ya kuondoshwa Ukuta wa Berlin
5 Februari 2009Novemba mwaka huo huo, ukuta wa Berlin uliotenganisha Ujerumani ya Mashariki na Magharibi uliangushwa na ukawa historia. Lakini miezi sita kabla, bado kulikuwepo amri ya kuwapiga risasi wakaazi wa Ujerumani ya Mashariki-DDR waliojaribu kukimbilia upande wa Magharibi.
Mnamo Februari 1989, kosa moja kubwa lilisababisha jeribio la kijana Chris Gueffroy kukimbilia upande wa Magharibi kwenda kombo.Askarijeshi mmoja aliekuwa rafiki yake alimuambia kuwa amri ya kuwapiga risasi wale wanaojaribu kukimbilia upande wa pili wa ukuta wa Berlin, imeondoshwa. Kijana Chris aliekuwa na umri wa miaka 20 alihisi kuwa hana uhuru huko DDR. Na kwa vile ulikaribia wakati wake kuandikishwa jeshini, yeye na rafiki yake waliamua kukimbilia magharibi kwa kuuchupa ukuta. Jioni ya February 5 mwaka 1989 vijana hao wawili walijificha katika bustani ndogo karibu na mpaka.Kwa kutumia ngazi tu walijaribu kuuparamia ukuta lakini kingóra kilianza kulia.
Baadae mashahidi upande wa Magharibi walisema, walisikia si chini ya milio kumi ya risasi na wakaona mtu akiondoshwa. Chris Gueffroy alifariki katika muda wa dakika chache na rafiki yake aliejeruhiwa vibaya alipelekwa jela.Siku mbili baadae ndio familia ya Chris iliarifiwa kuhusu kifo cha mtoto wao. Afisa wa askarikanzu alieleza kijuujuu tu kuwa kifo hicho kilitokea alipovamia eneo la kijeshi lililokuwa marufuku. Maziko ya kijana huyo yalihudhuriwa na watu wengi - miongoni mwao walikuwepo pia waandishi wa habari kutoka Magharibi. Jioni hiyo stesheni ya redio RIAS iliyokuwepo wakati huo Berlin ya Magharibi iliripoti hivi.
"Maelezo ya juu juu,jinsi kifo cha kusikitisha cha Chris kilivyotokea, yalikaririwa katika hotuba ya msimamizi wa maziko leo mchana.Hakuna zaidi kilichoelezwa rasmi kuhusu kile kilichosababisha kifo hicho.Makaburini walitawanywa askari wengi wa usalama tangu mapema.Baadhi ya askari kanzu walikuwepo hata katika ukumbi wa maombolezo."
Miezi sita baada ya kutokea kifo cha kijana huyo, DDR ilisambaratika. Mwanajeshi aliempiga risasi Chris,alifikishwa mahakamani mwanzoni mwa miaka ya tisini na akapewa kifungo cha jela cha miaka mitatu na nusu.Na serikali ya mwisho ya DDR ilipaswa kukubali jukumu la kutoa amri ya kupiga risasi. Egon Krenz akaadhibiwa kufungwa jela miaka sita na nusu.
Siku hizi watu na baiskeli hupita kule ambako Chris alijaribu kuchupa ukuta. Palipokuwepo ukuta sasa ni bustani na kumewekwa jiwe la kumbukumbu ya kijana wa mwisho aliepigwa risasi kwenye ukuta huo. Bunge la Ujerumani lilipendekeza kumbumbu hiyo na ikawekwa Juni 2003 ambapo angetimiza miaka 35.