1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kifo cha rais wa saba wa Ujerumani Roman Herzog

Oumilkheir Hamidou
11 Januari 2017

Kifo cha rais wa zamani waUjerumani Roman Herzog, uamuzi wa FIFA na wasichana wa Kiislam kutakiwa washiriki katika mafunzo ya kuogelea ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/2Vbuf
Altbundespräsident Roman Herzog - Amtseid
Picha: picture alliance/dpa/P. Grimm

Tunaanzia Berlin ambako kifo cha rais wa zamani wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani, mwanasheria aliyebobea aliyewahi kuwa rais wa korti kuu ya katiba, Roman Herzog kimewahuzunisha tangu wanaomjua mpaka wasiomjua. Ucheshi wake na mtindo wake wa kusema anachoamini ni cha maana mpaka leo unasifiwa. Gazeti la Badische Neueste Nachrichten linaandika: "Mojawapo ya hotuba zake imeingia katika madaftari ya historia ya Ujerumani aliposema malalamiko pekee hayasaidii kitu. Anaetaka kubadilisha kitu anabidi avinjari kweli kweli na aanze kwa kujitazama mwenyewe. Kama matamshi ya rais huyo wa zamani yamewaingia kweli kichwani wajerumani, kuna wanaoshuku. Daima watu wanapenda kuwanyooshea wengine kidole badala ya kujiangalia wao wenyewe wanafanya nini.

Hotuba inayolinganishwa na ile ya mapinduzi ya kiviwanda

 Gazeti la "Landeszeitung linaitaja hotuba hiyo kuwa ni ya kimapainduzi. Gazeti linaendelea kuandika: "Gazeti hilo la mjini Lüneberg linailinganisha hutuba ya Roman Herzog na aina mpya ya mapinduzi ya kiviwanda, hotuba inayohimiza maendeleo ya jamii katika enzi za utandawazi. Inahimiza ubunifu na kuamua juu ya mustakbal wa wajerumani. Ni hotuba ya aina yake kuwahi kutolewa Ujerumani na hata baada ya miaka 20 bado haikupoteza umuhimu wake.

Kuogelea ni sehemu ya mafunzo kwa wote,wasichana na wavulana

 Mvutano uliozuka kati ya baadhi ya familia za wahamiaji na shule kama wasichana wa kiislam washiriki au la katika mafunzo ya kuogelea umeshafumbuliwa. Mahakama ya Ulaya imebidi kuingilia kati, linaandika gazeti la Rhein-Necker-Zeitung: "Mafunzo ya pamoja ya kuogelea kati ya vijana wa kiume na wenzao wa kike yanahitaji uvumilivu na yanawapatia fursa wasichana wa kiislam ya kuuzoea mtindo wa maisha barani Ulaya. Kuangaliana  vijana wanapokuwa hawajavaa mashati ni sehemu ya mtindo huo na hilo linavumilika kwa sababu ni sehemu ya mafunzo. Kwa wasichana, bikini wanazoweza kuvaa katika vyoo vilivyotengwa kwa ajili yao tu, zinaweza kuwastiri mbele ya vijana wenzao wa kiume na hilo pia linaweza kuangaliwa kama ridhaa inayokubalika. Anaetarajia ukarimu anabidi pia achangie, la sivyo juhudi za kujumuishwa wahamiaji katika maisha ya kila siku ya jamii, haziwezi kufanikiwa.

Fifa yazidisha idadi ya timu

Mada yetu ya mwisho inahusu uamuzi wa shirikisho la kabumbu ulimwenguni FIFA kuzidisha idadi ya timu zitakazoshiriki katika fainali za kombe la dunia kuanzia mwaka 2026. Gazeti la Leipziger Zeitung linaandika: "Bado pengine chombo cha kujipatia fedha-yaani dimba, kinafanya kazi. Mpango wa kupanuliwa masoko hadi Asia na Afrika ndio kwanza unaanza. Kuzidisha idadi ya wadau si ishara nzuri. Kwa sababu fainali za kombe la dunia zinasisimua kutokana na kuretemka uwanjani timu bora za dunia na sio mpata mpatae. Kiwango cha dimba kikiporomoka, spoti ndio itakayoathirika. Na hasa dimba ambalo tayari limeshaingia madowa kutokana na kiu cha FIFA.

 

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir

Mhariri: Grace Patricia Kabogo