1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiir na Machar wakutana mjini Addis

21 Juni 2018

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na kiongozi wa waasi Riek Machar walikutana jana kwa mara ya kwanza tangu mwaka wa 2016, wakati ambapo muafaka wa Amani ulivunjika na mapigano yakazuka upya kati ya majeshi yao

https://p.dw.com/p/3008G
Südsudan Riek Machar  Salva Kiir
Picha: picture-alliance/AP/J. Patinkin

Machar ambaye alisalimiwa kabla ya mkutano huo na waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Ethiopia, Worken Gebeyehu, aliwasili Addis Ababa jana asubuhi. Kiir aliwasili mchana na kulakiwa na waziri mkuu Abiy.

Wigo wa mazungumzo rasmi ni mpana – kuzika tofauti kati ya viongozi hao wawili – lakini wachambuzi wanasema matokeo yake bado hayako wazi ikizingatiwa mahusiano tete kati ya watu hao wawili pamoja na misimamo yao mikali.

Maelfu ya watu wameuawa na karibu theluthi moja ya jumla ya idadi ya watu milioni 12 wamelazimika kuyakimbia makazi yao, na wengi wako ukingoni mwa kuangamia kutokana na baa la njaa.

Addis Abeba, Äthiopien, Äthiopischer Premierminister Abiy Ahmed im Parlament
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy AhmedPicha: DW/Y.Geberegziabher

Viongozi hao wawili wanaozozana walikwenda mjini Addis kutokana na mwaliko wa waziri mkuu mpya wa Ethiopia, Abiy, ambaye pia ni mwenyekiti wa jumuiya ya ushirikiano wa maendeleo wa nchi za Afrika Mashariki na pembe ya Afrika – IGAD ambayo imechukua usukani wa mazungumzo hayo ya Amani na ambayo mpaka sasa hayajazaa matunda.

Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Ethiopia Meles Alem amesema Waziri mkuu amewataka viongozi hao kupunguza tofauti zao na kushirikiana katika kurejesha utulivu Sudan Kusini na kuiondolea mzigo wa vifo na watu kukimbia nchini humo.

Viongozi wa serikali za IGAD wanatarajiwa kukutana leo mjini Addis, wakitumai kuyafufua mazungumzo ya Amani. Machafuko yaliyozuka upya yamesambaa kote nchini humo, na kuibua makundi mapya yenye silaha na kuuvuruga hata Zaidi mchakato wa Amani.

Afrika -Guinea Wurm
Maelfu ya Wasudan Kusini wamekimbia makaazi yaoPicha: picture-alliance/AP/M. Quesada

Mnamo mwezi Mei, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilizipa pande hizo mbili zinazozana mwezi mmoja kufikia muafaka wa Amani au wakabiliwe na vikwazo. Marekani ilikuwa muungaji mkono mkubwa wa Sudan Kusini  wakati ikijitenga kutoka Sudan, na inabakia kuwa mfadhili mkubwa wa misaada kwa nchi hiyo. lakini mapema mwezi huu, afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Marekanai alitishia kuziwekea pande zote za mzozo huo vikwazo baada ya ripoti moja kusema kuwa tabaka la juu la Wasudan Kusini linanufaika na ukiukaji wa haki za binaadamu.

Alan Boswell, mtafiti huru kuhusu taifa la Sudan Kusini, anasema mazungumzo ya sasa ndio jaribio la mwisho lakini muhimu la kufikia makubaliano. Anasema wasiwasi ni kuwa sio wazi kuhusu namna watakavyoepusha janga la mwaka wa 2016 kutokea tena, kwa sababu muundo wa muafaka huo sio tofauti na ulivyokuwa katika mkataba wa mwaka wa 2015.

Wanaharakati wameongeza sauti yao wakizitaka pande hizo mbili kufikia makubaliano endelevu ya Amani. Jukwaa la Asasi za Kiraia za Sudan Kusini limesema jana katika taarifa kuwa katika wakati huu muhimu ambao taifa na hali yake ya baadaye viko hatarini, viongozi hao wawili wanaozozana wana wajibu wa kimaadili na kisiasa wa kuungana pamoja na pia viongozi wengine nchini humo.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga