Kikao cha 12 cha AU chaingia siku yake ya mwisho
3 Februari 2009Mkutano huo unawaleta pamoja viongozi wa serikali na marais.Katika ufunguzi rasmi wa kikao hicho kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi aliteuliwa kuwa mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika.Wadhifa huo wa kupokezana unadumu kwa kipindi cha mwaka mmoja.Mwenyekiti wa zamani wa Umoja Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania alitoa shukrani zake kwa viongozi waliohudhuria kikao hicho vilevile kumpongeza Rais mpya wa Marekani Barack Obama.
Baadhi ya viongozi waliupongeza uteuzi wa Kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi.Kwa upande wake Muammar Gaddafi aliwahakikishia marais wenzake 20 waliokuwamo mkutano kwamba atatia juhudi zake zote ili kufanikisha hatua ya kuwa na Shirikisho la mataifa ya Afrika.Hata hivyo suala hilo limezua mitazamo tofauti na uamuzi kamili bado haujafikiwa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa upande wake alitilia mkazo umuhimu wa kutafuta suluhu za kikanda za migogoro inayokumba bara la Afrika vilevile changamoto za kusaka amani ya kudumu.Kiongozi huyo alitoa wito wa ushirikiano katika utatuzi wa migogoro hiyo.''Umoja wa Mataifa unatiwa moyo na juhudi za kikanda barani Afrika zilizo na uwezo mkubwa zaidi wa kufanikiwa ikilinganishwa na mapendekezo ya kuzuia ghasia yanayotokea Newyork.''
Nchi ya Somalia inayozongwa na migogoro ilipata rais mpya wiki iliyopita baada ya rais wa zamani Abdullahi Yusuf Ahmed kujiuzulu Disemba iliyopita.Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban ki Moon alimpongeza rais huyo mpya Sheikh Sharif Sheikh Ahmed na kusisitiza kuwa Umoja wa mataifa utaunga mkono juhudi za kusaka amani ya kudumu nchini humo.''Umoja wa Afrika utakuwa mstari wa mbele katika jitihada za kuimarisha ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM vilevile majeshi ya Somalia kwa ushirikiano na jamii ya kimataifa utahakikisha kuwa kuna nyenzo za kutosha''
Pembezoni mwa mkutano huo wa kilele Bwana Ban Ki Moon kadhalika alitoa wito kwa Rais wa Sudan Omar al Bashir kutoa ushirikiano kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita ICC iliyopendekeza hatua ya kumshtaki kwa tuhuma za uhalifu wa kivita uliotokea kwenye eneo la Darfur.Pendekezo hilo limepingwa vikali na baadhi ya viongozi barani Afrika.
Kulingana na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Jean Ping, Umoja huo huo unajitahidi kuwashawishi majaji kuupa muda wa miezi 12 mpango mzima wa kusaka amani ya kudumu nchini Sudan badala ya kuchukua hatua hiyo.
Wakati huohuo Umoja wa Ulaya uliahidi kuupa Umoja wa Afrika euro milioni 300 kwa minajili ya kufadhili operesheni za kulinda amani barani Afrika.Umoja wa Afrika unasimamia operesheni za kulinda amani katika nchi za Somalia,Sudan na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Suala la mgogoro wa Kongo nalo lilipongezwa baada ya nchi hiyo na jirani yake Rwanda kuanzisha operesheni ya pamoja ya kuwatimua waasi wa Rwanda wa kundi la FDLR katika eneo la Mashariki mwa Kongo.Mkutano huo wa kilele wa umoja wa Afrika unamalizika hii leo.
RTRE
APE