Kila mtoto yumo katika kitisho cha athari za kimazingira
19 Februari 2020Ripoti hiyo iliyopewa kichwa cha habari "Hatma ya watoto ulimwenguni" imetolewa na timu ya wataalamu zaidi ya 40 waliokusanywa na shirika la afya duniani WHO, shirika la kuwahudumia watoto UNICEF na jarida la masuala ya afya la Lancet. Kulingana na ripoti hiyo hakuna hata nchi moja duniani ambayo inakilinda kizazi kijacho kutokana na athari za uzalishaji wa gesi ya kaboni, uharibifu wa asili na ulaji wa vyakula vilivyosindikwa.
Profesa Anthony Costello kutoka taasisi ya afya ulimwenguni chuo kikuu cha London amesema ujumbe muhimu katika ripoti yao ni kwamba "hakuna nchi inayozingatia afya ya watoto sasa na hatma yao ya baadae" na kuongeza kwamba;
"WHO inaamini kuwa zaidi ya theluthi tatu ya vifo vya sasa vinatokana na athari za mazingira kwa watoto. Uchafuzi wa hewa, mtoto mmoja kati ya 10 havuti hewa safi, maji yasiyo salama ambayo tunafahamu ni mabaya kwa lishe na kiwango cha maambukizi."
Ripoti hiyo pia inaelezea kitisho kinachowakabili watoto kutokana na kutizama matangazo ya vyakula visivyo na afya, mafuta, sukari, pombe na tumbaku ambavyo vinahusishwa na unene uliopitiliza. Katika baadhi ya nchi watoto wanatizama matangazo hadi elfu 30 kwa mwaka.
Makampuni ya matangazo pia yanauza data kwa watoto zinazotokana na michezo ya elektroniki hadi kwa makampini makubwa ya teknolojia. Watafiti wanasema hofu kubwa ni jinsi matangazo ya kwenye mitandao ya kijamii namna inavyowalenga watoto kwa makusudi.
Watoto katika mataifa tajiri wana nafasi nzuri ya kuishi na kustawi. Mataifa kama Jamhuri ya Afrika ya Kati na Chad yanafana vibaya ukilinganisha na mataifa tajiri kama Norway na Uholanzi. Watoto pia huonyeshwa matangazo ya bidhaa yaliyokusudiwa watu wazima, kama vile pombe na tumbaku, na kuongeza nafasi ya utumiaji. Idadi ya watoto waliokuwa na unene wa kupitiliza ulimwenguni kote imefikia milioni 124.
Watoto karibu milioni 250 walio chini ya miaka mitano katika nchi za kipato cha kati wanakabiliwa na kitisho cha utapiamlo na athari nyinginezo za umaskini. Ripoti hiyo iliyochapishwa kwenye jarida la lancet imezipima nchi 180 katika vipengele vya maisha ya watoto, elimu na viwango vya lishe.