Kim atishia majaribio ya silaha kali, Trump ataka subira
1 Januari 2020Rais Trump ametumia salamu zake za Mwaka Mpya akiwa kwenye klabu yake ya Mar-a-Lago mjini Florida kuzungumzia imani na wasiwasi wake kwa kiongozi wa Korea Kaskazini, masaa kadhaa baada ya Kim kutangaza rasmi kuwa nchi yake haitajifunga tena na marufuku iliyojiwekea yenyewe ya kutofanya majaribio ya silaha za masafa marefu na za nyuklia.
"Kiongozi wa Korea Kaskazini alisaini makubaliano kuhusu kuindowa nchi yake kwenye mpango wa nyuklia na naamini ni mtu mwenye kuheshimu kauli yake," alisema Trump mbele ya waandishi wa habari, akiongeza kwamba "Kim alisaini makubaliano hayo nchini Singapore."
Katika hotuba yake mbele ya mkutano mkuu wa chama tawala cha Wafanyakazi, Kim alisema kwamba nchi yake inapanga kuendeleza mpango wake wa nyuklia, kuanzisha kile alichokiita "silaha ya kimkakati", licha ya kuendelea kuahidi kwamba yuko tayari kwa mazungumzo na Marekani, ambayo "imedharau muda wa mwisho wa kufufuwa mazungumzo" baina yao.
Kikao hicho cha ngazi za juu kilifanyika kwa siku nne mfululizo kuelekea siku ya mwisho ya mwaka 2019, ambayo Kim aliiwekea Marekani iwe imesharidhia matakwa ya Korea Kaskazini kabla ya kurejea kwenye meza ya mazungumzo. Marekani inasema muda huo wa mwisho uliowekwa na Korea Kaskazini haukuwa sahihi.
Kim aapa kurejea kwenye mpango wa nyuklia
Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Korea Kaskazini, KCNA, Kim aliwaambia wajumbe wa mkutano huo wa ngazi za juu kabisa kwamba nchi yake "haikuwa na haja ya kuendelea kujifunga na marufuku iliyojiwekea yenyewe dhidi ya kufanya majaribio ya silaha za nyuklia na makombora ya masafa marefu."
Kim aliishutumu Marekani kwa kuja na "matakwa ya kihuni" na kuendelea kushikilia "sera za kihasama", ikiwemo kufanya mazoezi ya kijeshi na Korea Kusini, kutumia silaha kali na kuiwekea nchi yake vikwazo.
Aliahidi kuendelea kuimarisha mpango wa nyuklia wa nchi yake na kusema kwamba kina na wigo wa mpango huo "kitaamuliwa kutokana na hulka ya Marekani."
"Dunia itashuhudia silaha mpya ya kimkakati ikimilikiwa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea hivi karibuni," alisema Kim akitumia jina rasmi la Korea Kaskazini.
"Tutaendeleza kwa uhakika uwezo wetu wa kinyuklia ili kukabiliana na kitisho cha nyuklia kutoka Marekani na kuhakikisha usalama wetu wa muda mrefu."
Korea Kaskazini imekuwa ikirusha makombora ambayo yana uwezo wa kufika popote ndani ya ardhi ya Marekani, na imeshafanya majaribio sita ya nyuklia na wachambuzi wanasema tamko hilo la Kim ni sawa na kumtupia kombora Rais Trump.
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Mike Pompeo, aliita kauli hiyo ya Kim kuwa ya kuudhi na kuvunja moyo.