1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kim Jong Un ameiomba msamaha Korea ya Kusini

Saleh Mwanamilongo
25 Septemba 2020

Kiongozi  wa Korea kaskazini  Kim Jong Un  ameomba  radhi  baada ya wanajeshi  wa nchi yake kumpiga risasi na kumuua  afisa wa wizara kutoka Korea kusini.

https://p.dw.com/p/3j10K
Südkorea  WSFMS Fischfang Ministerium Flotte
Picha: Yonhap/picture-alliance

Kiongozi  wa Korea  kaskazini  Kim Jong Un  ameomba  radhi  leo baada ya wanajeshi  wa nchi yake kumpiga risasi na kumuua  afisa wa wizara kutoka Korea kusini karibu na  mpaka  wa baharini  wa nchi hizo mbili. 

Shirika la habari la Korea kusini  limeripoti kuwa katika  ujumbe  wake  Kim Jong Un, amesema  amesikitishwa mno kwamba amemvunja  moyo rais wa Korea  kusini Moon Jae In, likinukuu taarifa  kutoka  ofisi  ya  rais.

Suh Hoon,mshauri wa baraza la usalama wa Taifa ,Korea ya Kusini  alisoma barua kutoka kwa chama tawala cha Korea ya Kaskazini inayosema serikali ya  Pyong Yang imekiri kufyetuwa risasi zaidi ya kumi kwa mtu huyo aliyeingia kinyume cha sheria kwenye eneo la maji  yake na ambaye alikataa kujitambulisha.

''Rais Kim Jong Un ametuambia katika ujumbe wake kwamba amesikitishwa na tukio hilo na kusema pahali pa kusaidia raia wa Korea ya Kusini wanaotaabika na tishio la ugonjwa wa Corona, kumetokea kwenye eneo la maji yetu tukio lisilotarajiwa na la aibu, ambalo limewasikitisha rais Moon na raia wake wa Korea ya Kusini.'',alisema Hoon.

Barua hiyo inasema walinzi wa mipaka wa Korea ya Kaskazini walimuua kufuatia amri walizopewa.

Suh Hoon,mshauri wa baraza la usalama wa Taifa nchini Korea ya Kusini.
Suh Hoon,mshauri wa baraza la usalama wa Taifa nchini Korea ya Kusini.Picha: Yonhap/picture-alliance

Ijumaa serikali ya PyongYang haikuthibitisha uwepo wa barua hiyo na vyombo vya habari vya Korea ya Kaskazini havikuripoti kuhusu tukio hilo.

Matumaini ya maridhiano baina ya Kim na Moon

Wadadisi wanaelezea kwamba kufuatia ujumbe huo, Korea ya Kaskazini inajaribu kutumtuliza jirani wake wa Kusini,ambako mauwaji hayo ya kwanza kufanywa na jeshi  la Korea Kaskazini mnamo kipindi cha miaka 10,yalizusha mhemuko.

Ahn Chan-Il, aliyetoroka Korea ya Kaskazini na ambaye amefanya utafiti mjini Seoul, amesema kwamba  ni nadra sana kiongozi wa Korea ya Kaskazini kuomba msamaha kwa Korea ya Kusini.

Leif Eric Easley, Profesa kwenye chuo kikuu cha Ewha, mjini Seoul amesema  Kim Jong Un kuomba msahama  kunapunguza athari za kuweko na makabiliano baina ya nchi mbili hizo na kuwepo na matumaini ya maridhiano na rais Moon.

Wanajeshi  walimpiga  risasi  mtu  huyo siku  ya  Jumanne, kwa sababu walifikiri  kuwa  ni mvamizi. Wizara ya  ulinzi  ya  Korea  kusini  ilisema hapo  kabla  kuwa  afisa  huyo mwenye umri wa miaka 47, na mfanyakazi wa  wizara inayoshughulikia masuala ya bahari na  uvuvi ya Korea  kusini, alitoweka kutoka  katika  boti wakati  akiwa  katika ujumbe  wa  ukaguzi kiasi  ya  kilometa 10 kusini mwa  mpaka  wa  baharini  na  Korea kaskazini.

Baadaye mwili wa afisa huyo uliosalia kwenye maji,aminika kuchomwa moto na wanajeshi wa Korea ya Kaskazini kwa hofu ya maambukizi ya virusi vya Corona.