Kim Jong Un asifu utulivu Rasi ya Korea
19 Septemba 2018Kim alitoa matamshi hayo wakati wa mkutano wa kilele na Rais Moon Jae-in wa Korea Kusini katika mji mkuu wa Korea Kaskazini, Pyongyang, siku ya Jumanne (tarehe 18 Septemba).
Moon alikuwa ziarani mjini Pyongyang na Kim alisema kuwa anafurahishwa na jinsi hali ya kisiasa ilivyotengamaa kwenye kanda hiyo siku za hivi karibuni miezi kadhaa tangu mkutano wake na Rais Trump.
Kim alisifu nafasi muhimu ya upatanishi iliyoratibiwa na Moon Jae-in katika kufanikisha mazungumzo ya mwezi juni nchini Singapore na Rais Trump ambapo viongozi hao walikubaliana kuweka mipango ya kuondoa kitisho cha silaha za kinyuklia katika Rasi ya Korea.
Kwa upande wake, rais wa Korea Kusini alimshukuru Kim kwa hotuba yake aliyoitoa mwanzoni mwa mwaka mpya iliyofungua milango ya utengamano na baadaye kutuma ujumbe wa ngazi ya juu wa serikali yake kwenda Korea Kusini wakati wa Michezo ya Olimpiki ya msimu wa baridi mwezi Februari mwaka huu.
Matokeo ya mkutano bado hayajatolewa
Mkutano huo uliofanyika katika jengo la makao makuu ya Chama Cha Kisoshalisti cha Korea Kaskazini ulihudhuriwa pia na maafisa wa ngazi ya juu wa serikali zote mbili ambapo rais wa Korea Kusini alifuatana na mkuu wake wa ujasusi Suh Hoon na mkurugenzi wa ulinzi wa rais Chung Eui-yong.
Kwa upande wake Kim aliambatana na dada yake mwenye ushawishi mkubwa Kim Yo Jong na kiongozi mwandamizi wa chama cha wafanyakazi cha Korea Kaskazini Kim Yong Chol.
Hadi sasa lakini hakuna taarifa kamili ya matokeo ya mkutano huo iliyotolewa.
Mkutano mwengine umepangwa kufanyika hapo siku ya jumatano ingiwa hapajawa na maelezo yoyote juu ya iwapo viongozi hao wawili watachapisha taarifa ya pamoja ya makubaliano ya mazungumzo hayo.
Nyuklia ajenda kuu ya mkutano
Moon, ambaye amekuwa mpatanishi katika mazungumzo kuhusu silaha za nyuklia kati ya washington na Pyongyang alisema jana kuwa atatafuta suluhu ya kudumu juu ya suala hilo wakati wa ziara yake ya siku tatu nchini korea kaskazini
Kim Jong Un alitangaza azma yake ya kuondoa silaha za nuklia kwenye rasi ya Korea mapema mwezi Aprili na Mei na pia wakati wa mkutano wake wa kihistoria na rais wa marekani Donald trump nchini Singapore mwezi Juni mwaka huu.
Hata hivyo matamshi yake hayakutoa maelezo kamili ya ni lini na kwa namna gani mpango huo utakamilika na Washington hivi sasa imesema hairidhishwi na jinsi nchi hiyo inatekeleza makubaliano ya kuikongoa mifumo yake ya uundaji silaha za nyuklia na ingependelea kuona ahadi zinazotimizwa
Mwandishi: Rashid Chilumba/AFP/AP/APTN
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman