1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kim Jong Un kukutana na rais wa Korea Kusini Moon Jae-in

Isaac Gamba
29 Machi 2018

Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, atakutana katika mkutano wa kilele na Rais wa Korea Kusini, Moon Jae-in, utakaofanyika kwenye kijiji cha mpakani cha Panmunjom mwishoni mwa mwezi ujao.

https://p.dw.com/p/2vAue
Nordkorea Führer Kim Jong Un
Picha: picture-alliance/AP Photo/Wong Maye-E

Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja nchi hizo mbili zinapanga kuwa na kikao kingine Aprili 4 cha kuandaa mkutano huo wa kilele wa Aprili 27, ikiwa ni pamoja na  kujadili itifaki, usalama na jinsi vyombo vya habari vitakavyoripoti mkutano wa kilele ambao utakuwa wa kwanza wa aiana yake kufanyika baada ya miongo kadhaa.

Viongozi wa nchi hizo mbili wamekuwa na mazungumzo mara mbili tu tangu vita vya Korea vya mwaka 1950-53 ambapo walikutana mjini Seoul mwaka 2000 na 2007 chini ya serikali za wakati huo za kiliberali.

Rasi ya Korea iligawanywa pande mbili mwaka 1945 ambapo upande wa kusini ulidhibitiwa kwa kiwango kikubwa na  Marekani huku Urusi ikunga mkono upande wa Kaskazini.

Waziri wa Korea Kusini anayehusika na masuala ya muungano, Cho Myoung-gyon, ambaye ni miongoni mwa maafisa wa Korea Kusini walioshiriki mazungumzo yaliyofanyika leo Alhamisi, amewaeleza waandishi wa habari kuwa suala la kupanga majadiliano kati ya viongozi wa nchi hizo mbili katika kutafuta njia za kuishawishi Korea Kaskazini kuachana na mipango yake ya silaha za nyuklia itakuwa ni ajenda muhimu.

 

Kikao cha maandalizi chafanyika

Südkorea PK Moon Jae-in
Rais wa Korea Kusini Moon Jae-inPicha: Reuters/Jung Yeon-Je

Ujumbe wa maafisa watatu wa Korea Kaskazini walishiriki katika kikao hicho kilichofanyika leo kupanga tarehe ya mkutano wa kilele pamoja na masuala mengine uliongozwa na mwenyekiti wa taasisi ya nchi hiyo inayohusika na masuala ya Korea Kaskazini na Korea Kusini, Ri Son Gwon.

Nchi hizo mbili mapema mwaka huu zilifikia makubaliano kwa ajiili ya mkutano wa kilele utakaofanyika  upande wa kusini wa kijiji cha mpakani.

Akisalimiana na maafisa wa Korea Kusini kwenye jengo linalodhibitiwa na Korea Kaskazini, Ri ameelezea matumaini ya kupatikana matokeo mazuri yanayotarajiwa  huku waziri wa Korea Kusini anayehusika na masuala ya muungano akisema maafisa katika mkutano huo wa maandalizi watapaswa kufanya kila wanaloweza kufanikisha mkutano huo wa kilele kutokana na  kuwa hali iliyofikiwa hivi sasa imechangiwa kikubwa na maamuzi yaliyofanywa na viongozi wa juu wa nchi hizo mbili.

Mazungumzo hayo yanafuatia mkutano wa kushitukiza wiki hii kati ya Kim Jong wa Korea Kaskazini na Rais wa China, Xi Jinping, ambao ulionekana kuboresha misimamo ya nchi zote mbili kabla ya Kim Jong Un kukutana na Rais Moon wa Korea Kusini na pia Rais Donald Trump wa Marekani.

Mwandishi: Isaac Gamba/APE/DW

Mhariri: Mohammed Khelef