Kim Jong Un kukutana na Trump
9 Machi 2018Akiwa amesimama nje ya Ikulu ya White House, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Korea Kusini Chung Eui-yong alitangaza kuhusu mkutano wa kwanza kabisa kuwahi kufanyika kati ya rais wa Marekani na Kiongozi wa Korea Kaskazini, ambao alisema utafanyika mwishoni mwa Mei. KIM EUI-KYEOM ni msemaji wa rais wa Korea Kusini.
Trump alisifu hatua kubwa zilizopigwa katika kuishinikiza Korea Kaskazini kuumaliza mpango wake wa nyuklia, lakini amesisititiza kuwa vikwazo vitaendelea kuwekwa. Ijapokuwa Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence alisema msimamo wa Marekani kuelekea Korea Kaskazini hautabadilika hadi pake watakapoona hatua za kweli, zinazoweza kuthibitishwa na imara kuelekea katika usitishwaji wa mpango wa nyuklia.
Habari hizo zimetolewa baada ya kipindi cha mvutano mkali kati ya Marekani na Korea Kaskazini ambao wakati mwingine ulionekana kama ni dalili za kuzuka vita. Ikulu ya White House imesema katika taarifa kuwa mkakati wa shinikizo la juu litaendelea kutumiwa.
China imelikaribisha tangazo hilo huku ikiwataka Trump na Kim kuonyesha ujasiri wa kisiasa katika kuondoa silaha za nyuklia katika rasi ya Korea.
Japan, mshirika muhimu wa kikanda, imesifu tangazo hilo la kuandaliwa mkutano wa kilele ambao imesema ni nguzo ya kusaidia kuwachana na utengenezaji wa silaha za nyuklia, lakini ikasema haitaacha kuiwekea Pyongyang shinikizo la kidiplomasia. Shinzo Abe ni Waziri Mkuu wa Japan. Korea Kusini pia imetangaza kuwa Korea hizo mbili zitaandaa mwezi ujao mkutano wa kilele wa kihistoria katika ukanda wa mpakani usio na shughuli za kijeshi
Rais wa Korea Kusini Moon Jae in alielezea furaha yake akisema mkutano huo wa mwezi Mei utaandikishwa kuwa hatua ya kihistoria ambayo ilileta Amani katika Rasi ya Korea.
Lakini wachambuzi wanaikosoa kabisa hatua hiyo, wakisema mkutano wa kilele kati ya Marekani na Korea Kaskazini ni ushindi kwa Kim. Evan Medeiros kutoka shirika la Eurasia Group, na mshauri wa zamani wa Barack Obama, anasema mkutano huo unampa Kim hadhi sawa na rais wa Marekani na unaimarisha jaribio lake la kutaka Korea Kaskazini kutambulika kama dola la kinyuklia.
Anasema hautaifanya Korea Kaskazini kuwachana na silaha za nyuklia. Badala yake, itaimarisha hadhi yake na uhalali wa utawala wa Kim, kumpa muda zaidi wa kutengeneza silaha zake za nyuklia na kumuwezesha kutapa nafasi ya kutaka aondolewe vikwazo
Jeffrey Lewis, kutoka Taasisi ya Middlebury ya Masomo ya Kimkakati anasema Trump anaucheza muziki wa Kim. Anasema Kim hajamwalika Trump ili kuzisalimisha silaha za nyuklia za Korea Kaskazini, bali anamualika kumuonyesha kuwa uwekezaji wake katika uwezo wa nyuklia na makombora umeilazimu Marekani kumchukulia kuwa kwa kiwango sawa.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Grace Patricia Kabogo