1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kim kufunga mitambo ya nyuklia mbele ya waangalizi wa kigeni

Sylvia Mwehozi
19 Septemba 2018

Korea Kaskazini imesema siku ya Jumatano kwamba itaifunga mitambo yake muhimu ya makambora mbele ya uangalizi wa wataalamu wa kimataifa, ishara ya karibuni ya kiongozi Kim Jong Un ya kufufua mazungumzo yake na Marekani.

https://p.dw.com/p/358nJ
Nordkorea - Korea-Gipfel in Pjöngjang: Kim Jong Un trifft Moon Jae-In
Picha: Getty Images/Pyeongyang Press Corps

Wakizungumza katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari mjini Pyongyang, Kim na rais wa Korea Kusini Moon Jae-in wamesema wamekubaliana kuigeuza rasi ya Korea kuwa "eneo la amani bila ya silaha na vitisho vya kinyukilia". Wamesema Korea kaskazini pia imedhamiria kuufunga mtambo wake mkuu wa nyukilia kama Marekani itachukua hatua zilizo sawa.

"Tumekubali makubaliano ya kijeshi ili kukomesha historia ya mapambano ya ukatili na mabaya na uadui, na kukubaliana kufanya jitihada za kuirejesha rasi ya Korea kuwa eneo la amani bila silaha za nyuklia na vitisho vya nyuklia," alisema kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong Un 

Naye rais wa Korea Kusini Moon Jae-in amesema kwamba. "Wananchi wa Korea kaskazini na Kusini. Rasi ya Korea bila ya vita imeanza. Korea kusini na kaskazini zimekubaliana leo kuondoa kitisho chochote kilichopo katika rasi ya Korea ambacho kinaweza kusababisha vita. Tumekubaliana kuanzisha tume ya pamoja ya kijeshi itakayofanya majadiliano ya kila mara ili kufikia makubaliano ya kijeshi".

Nordkorea Moon Jae In, Präsident Südkorea & Kim Jong Un in Pjöngjang
Rais wa Korea Kusini na kiongozi wa Korea Kaskazini wakionyesha makubaliano waliyofikiaPicha: picture-alliance/dpa/KBS via APTN

Ahadi za Kim na Moon zilizotolewa katika mkutano wao wa tatu wa kilele kwa mwaka huu zinaweza kuongeza kasi mpya katika mazungumzo ya nyuklia yalokwama kati ya Korea Kaskazini na Marekani na kuweka msingi wa mkutano mwingine na rais Donald Trump uliopendekezwa hivi karibuni na Kim.

Kim ameahidi kufanyia kazi kuelekea "kumaliza kikamilifu shughuli za nyukilia katika rasi ya Korea", wakati alipokutana na Moon mapema mwaka huu na wakati wa mkutano wa kihistoria na Trump mjini Singapore.

Lakini mjadala wa jinsi gani ya kutekeleza ahadi hizo zisizo wazi umetawala tangu wakati huo. Washington inahitaji hatua kamilifu juu ya kumalizwa kwa shughuli za nyukilia, kama vile kufungwa kwa miundombinu ya Korea Kaskazini ya nyukilia na makombora, kabla ya kukubaliana na malengo muhimu ya Pyongyong, kutangaza mwisho rasmi wa vita ya Korea ya mwaka 1950-53  na kuondokana na vikwazo vikali vya kimataifa.

Nordkorea Moon trifft zu drittem Korea-Gipfel in Pjöngjang ein
Viongozi wa mataifa mawili ya Korea wakikumbatiana huku wake zao wakisalimianaPicha: Getty Images/Pyeongyang Press Corps

Rais wa Marekani Donald Trump kupitia ukurasa wake wa Twitter amesifu ahadi hizo akisema ni za "kusisimua sana".

"Kim Jong Un amekubali kuruhusu ukaguzi wa nyukilia, kulingana na makubaliano ya mwisho na kuharibu kabisa mtambo wa majaribio mbele ya wataalamu wa kimataifa. Wakati huo hakutakuwa na roketi au majaribio ya kinyukilia".

Kim amesema atazuru Seoul katika siku za usoni, ziara ambayo inaweza kuwa ya kwanza na aina yake kufanywa na kiongozi wa Korea kaskazini. Moon amesema ziara hiyo inatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu. Viongozi hao wa mataifa mawili ya Korea pia walitangaza mfululizo wa hatua za kuimarisha ushirikiano wa nchi mbili katika nyanja za kiuchumi, kitamaduni na michezo.

Ahadi hizo za Kim zinakuja siku chache kabla rais wa Korea Kusini Moon Jae-in hajakutana na Trump jijini New York, pembezoni mwa mkutano mkuu wa Umoja wa mataifa utakaofanyika wiki ijayo. Maafisa wa Seoul wana matumaini kwamba Moon ataweza kumshawishi Trump kuanzisha mazungumzo ya nyukilia na Pyongyang, baada ya kufuta ziara ya waziri wake wa mambo ya kigeni mjini humo mwezi uliopita kwa madai kuwa hakuna hatua zilizokwisha pigwa.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman