Kimbele mbele cha Saud Arabia,London na Incirlik Magazetini
6 Juni 2017Tunaanza na hatua zilizochukuliwa na baadhi ya nchi za kiarabu dhidi ya Qatar. Gazeti la "Südwest Presse" linaandika: "Wasuudi na vibaraka wao katika baraza la ushirikiano la nchi za Ghuba wamemuelewa rais mchangamfu wa Marekani kana kwamba wakati umewadia sasa wa kuundwa kambi ya nchi za kiarabu na Marekani dhidi ya Iran na kulipiza kisasi dhidi ya wanaopotoka. Ingwa ni kweli kabisa kwamba nchi hiyo tajiri kupita kiasi ya Qatar inawaunga mkono kifedha magaidi, lakini hata Saud Arabia na Kuweit wanafanya hivyo hivyo. Nadharia ya ukatili ya wahabbi inatekelezwa sio tuu kwa fedha za mafuta ya Qatar bali pia za Saudia na Kuweit. Si hasha kwa hivyo kuona kimbele mbele cha Saud Arabia kikiwadhuru wenyewe."
Sasa basi ifuatwe na vitendo kuondowa hofu za wananchi
Mashambulio yaliyoutikisa mji mkuu wa Uingereza London na kuangamiza maisha ya watu wasiopungua saba yangali bado yanagonga vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani. Gazeti la kaskazini mwa Ujerumani "Hannoversche Allgemeine" linaandika:"Kauli moja tu ndiyo iliyosikika mnamo wiki endi ya Pantekoste: "Basi sasa". Kauli hiyo ameitamka waziri mkuu wa Uingereza Theresa May mnamo siku ya pili ya shambulio la kigaidi- la kikatili kupita kiasi lililotokea hivi karibuni mjini London. Kauli hiyo ni bayana-inamaanisha "wakati wa matamshi umekwisha."Hata hivyo kauli hiyo inadhihirisha pia mbinu ya mwanasiasa anaendesha kampeni ya uchaguzi kutaka kuonyesha anaidhibiti hali ya mambo. Maarifa yote kuhusu magaidi yanaonyesha , mbali na msimamo mkakamavu na ushupavu, daima linaibuka suala kuhusu chanzo cha magaidi. Kauli ya "Basi sasa" pengine inatosha kutuliza nyoyo za watu kwa muda mfupi, lakini utaratibu madhubuti wa kuwaondolewa watu hofu, tija yake ni ya muda mrefu."
Dawa ya Uturuki ni kuondolewa wanajeshi wa Ujerumani toka Incirlik
Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu mvutano kati ya Uturuki na Ujerumani baada ya viongozi wa mjini Ankara kuwakatalia ruhusa wabunge wa Ujerumani kuwatembelea wanajeshi wao waliowekwa katika kituo cha jeshi la wanaanga la Incirlik. Gazeti la "Trierischer Volksfreund" linaandika kuhusu ziara iliyofanywa na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel mjini Ankara. "Serikali kuu ya Ujerumani haikubakisha juhudi za kidiplomasia. Sasa basi tena. Ikiwa Uturuki inashikilia uzi ule ule, inawakatalia wabunge wa Ujerumani ruhusa ya kwenda kuwatembelea wanajeshi wa Ujerumani huko Incirlik, basi jibu ni moja tu, wanajeshi hao waondishwe Uturuki. Hapo viongozi wa Ankiara hawatowazungusha tena viongozi wa serikali kuu ya Ujerumani.
Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Iddi Ssessanga