1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kimbunga Kenneth kusababisha maafa zaidi nchini Msumbiji

Sylvia Mwehozi
26 Aprili 2019

Kimbunga Kenneth kimepiga pwani ya kaskazini ya Msumbiji usiku wa Alhamis huku mvua kubwa zikitarajiwa mara mbili zaidi ya dhoruba iliyoupiga mji wa Beira mwezi uliopita. Mtu mmoja amefariki huku makazi yakiharibiwa. 

https://p.dw.com/p/3HUKF
Mosambik, Moroni: Tropensturm Kenneth
Picha: Getty Images/AFP/I. Youssouf

Kimbunga Kenneth kimelipiga jimbo la Cabo Delgado, kisha baadae kikaelekea jimbo la Sofala kaskazini mwa Msumbiji ambako ndiko uliko mji wa Beira ulioathiriwa zaidi na kimbunga Idai mwezi uliopita. Kimbunga Idai kiliwaua mamia ya watu na kusababisha maelfu kukosa makazi nchini Msumbiji, Malawi na Zimbabwe.

Kwa mujibu wa shirika la Mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa WFP, kimbunga Kenneth kinatarajiwa kusababisha mvua kubwa katika kipindi cha siku 10 zijazo ikiwa ni mara mbili zaidi ya zile zilizonyesha wakati wa kimbunga Idai. Katika taarifa yake WFP imesema wilaya nne za Cabo Delgado za Macomia, Mocimboa da Praia, Muidumbe na Palma, zinatazamiwa kuathirika zaidi kutokana na upepo unaotarajiwa kupiga kwa zaidi ya kilometa 120 kwa saa. Kwa mujibu wa WFP, kiasi ya watu 112,000 wako hatarini na kwamba shirika hilo lina zaidi ya tani 1,000 za msaada wa chakula tayari kuwasaidia watakoathirika.

Serikali ya Msumbiji imeanza kuwalazimisha watu kuondoka katika maeneo yaliyoko hatarini siku mbili kabla ya kimbunga kupiga. Jumla ya watu 30,000 wamehamishiwa katika maeneo salama, huku shule zikitumika kuwahifadhi watu hao. Rais Filepe Nyusi amewahutubia wananchi kupitia televisheni akiwataka kuwa watulivu. Kimbunga hicho pia kilisababisha maafa katika visiwa vya Comoro. Mkurugenzi mkuu wa ulinzi wa kiraia visiwani humo Ismael Mogne Daho, amethibitisha vifo vya watu watatu. Mmoja wa wakazi wa visiwani humo aliyeathirika anasema.

Archipel der Komoren/Anjouan | Zyklon Kenneth in Comoros
Athari za kimbunga Kenneth kisiwani Anzuan, ComoroPicha: picture-alliance/dpa/ZUMAPRESS/Le Pictorium Agency/N. Beaumont

''Usiku ulikuwa wa hofu sana matumboni mwetu. Kuanzia saa nne usiku na kuendelea, hatukulala. Hali ya hewa ilikuwa mbaya sana na hatukujua wapi pa kwenda katika kiza cha namna ile na watoto. Mvua kubwa ilinyesha na upepo mkali. Miti ilianguka, hapo palikuwa na muembe, tulikuwa tukikaa chini yake lakini uliangushwa''. 

Soma Zaidi...

Mkuu wa shirika la misaada ya kiutu la Umoja wa Mataifa OCHA, Mark Lowcock amesema upepo unaotokana na kimbunga Kenneth umefikia kilometa 270 kwa saa na kusababisha "mafuriko makubwa'. Naye naibu mkurugenzi katika taasisi ya kupambana na maafa ya Msumbiji Antonio Beleza amesema mapema leo kuwa asilimia 90 ya nyumba katika kisiwa cha Ibo mjini Cabo Delgado zimeharibiwa na dhoruba.

Mwanamke mmoja ameripotiwa kupoteza maisha katika mji wa Pemba kaskazini mwa Msumbiji baada ya kuangukiwa na mti kutokana na kimbunga Kenneth huku nyumba zikiharibiwa. Tahadhari ya kutokea kimbunga Kenneth ilitolewa pia na mamlaka ya hali ya hewa nchini Tanzania TMA, hususan katika maeneo ya mji wa kusini wa Mtwara. Serikali mjini humo jana iliwaamuru wanafunzi na wafanyakazi kubakia majumbani..dpa/ap