Kimbunga Matthew chawaua watu 300 Haiti, chawasili Marekani
7 Oktoba 2016Maafisa wa Haiti wamesema zaidi ya watu 339 wameuawa na kimbunga hicho, maelfu wameachwa bila ya makaazi na miundo mbinu imeharibiwa vibaya mno hasa eneo la kusini magharibi mwa nchi hiyo huku idadi ya walioathirika ikitarajiwa kuongezeka.
Maafa ya kimbunga hicho yamesababisha uchaguzi mkuu uliokuwa ufanyike Jumapili hii kuahirishwa. Katika nchi jirani, Katika Jamhuri ya Dominican watu wanne pia walikufa.
Kimbunga Matthew kinatajwa kuwa kibaya zaidi kuikumba Marekani na nchi za Carribean katika kipindi cha miaka kumi iliyopita. Upepo mkali unaovuma kwa kilomita 230 kwa saa na mvua kubwa zimeripotiwa katika miji ya pwani ya Florida huku kimbunga hicho hatari ambacho kimeorodhoshwa katika kiwango cha nne kikisababisha kutangazwa hali ya tahadhari katika majimbo kadhaa.
Kulingana na gavana wa Florida Rick Scott, zaidi ya nyumba 140,000 za Florida hazina umeme. Scott amewahimiza raia wa jimbo lake kuitikia mwito wa kuyahama makaazi yao kabla hawajakumbwa na maafa.
Licha ya kuwa kufikia leo asubuhi nguvu ya kimbunga Matthew ilishuka hadi kiwango cha tatu, kituo cha utabiri wa hali ya hewa cha Marekani kimeonya kuwa bado kuna hatari ya maafa makubwa.Idara ya utabiri wa hali ya hewa imesema kimbunga hicho huenda kikawa kibaya zaidi kuikumba kaskazini mashariki ya jimbo hilo la Florida katika kipindi cha miaka 118.
Bado ni mapema kutabiri ni kwa kiasi gani kimbunga hicho kitayaathiri majimbo ya Georgia, Florida, South na North Carolina lakini tayari kiasi cha watu milioni 12 wamewekwa katika hali ya tahadhari huku watu milioni tatu wakihamishiwa maeneo salama.
Barabara katika majimbo hayo yamekumbwa na msongamano mkubwa wa magari na vituo vya kujazia mafuta na maduka ya vyakula yakiishiwa bidhaa, kila mmoja akijaribu kuwekeza akiba kabla ya kimbunga kufika katika maeneo yao. Maelfu ya safari za ndege pia zimefutiliwa mbali.
Rais wa Marekani Barack Obama aliwapigia simu magavana wa majimbo hayo kujadili mikakati iliyowekwa kukabiliana na kimbunga hicho na kutangaza hali ya hatari katika majimbo ya Florida na South Carolina pamoja na kutangaza hali ya tahadhari Georgia.
Kituo cha kutabiri vimbunga Marekani NHC, kimesema kimbunga Mathew kinatarajiwa kuendelea kuvuma Alhamisi na Ijumma lakini kinabashiriwa kuanza pole pole kupotea nguvu katika kipindi cha saa 48 zijazo.
Mwandishi: Caro Robi/Reuters/dpa
Mhariri:Iddi Ssessanga