1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kimbunga Sally chasababisha mafuriko nchini Marekani

17 Septemba 2020

Mtu mmoja amefariki na majengo 550,000 katika majimbo ya Alabama, Florida na Mississippi kukatikiwa umeme. Kikosi cha ulinzi wa taifa kimetuma wanajeshi 200 katika jimbo la Alabama kusaidia katika juhudi za uokoaji.

https://p.dw.com/p/3icof
Hurrikan Sally
Picha: picture-alliance/AP Photo/NOAA

Kituo cha kitaifa cha kushughulikia masuala ya vimbunga NCH, kimesema Kimbunga Sally kiliwasili katika Pwani ya Alabama nchini Marekani mapema Jumatano asubuhi. Kituo hicho cha NHC pia kimethibitisha kufariki kwa mtu mmoja na kunyesha kwa mvua kubwa huku maji ya bahari yakiongezeka na kuhofiwa kusababisha mafuriko makubwa katika siku zijazo.

Kimbunga hicho cha kategoria ya pili kilikuwa cha kasi ya kilomita 5 kwa saa na kupiga ghuba hiyo ya Pwani kwa upepo wa kasi ya kilomita 165 kwa saa.

Kituo cha NHC kimesema maeneo ya Pwani ya majimbo ya Alabama, Mississippi na Florida yanakabiliwa zaidi na hatari ya uharibifu kutoka kwa kimbunga hicho na kwamba baadhi ya maeneo yaliotengwa yana uwezo wa kupokea mvua ya takriban futi tatu. Kimbunga hicho kilisababisha maporomoko ya ardhi karibu na fukwe za ghuba hiyo na kuelekea kwa haraka katika maeneo ya Pensacola, Florida, Alabama na maeneo ya mji mkuu yalio na takriban wakazi milioni 1 kwa ujumla.

Meya wa jimbo la Alabama Toy Kennon ameliambia shirika la habari la Ufaransa  AFP kwamba kifo kilichotokea kilitokea katika ufukwe wa bahari ya Orange jimboni humo na kwamba mtu mmoja bado hajulikani alipo. Kennon ameongeza kuwa takriban watu 50 katika ufukwe huo wa bahari ya Orange waliokolewa kutoka amakazi yao yaliokumbwa na mafuriko na kupelekwa katika maeneo salama.

Tovuti ya poweroutage.us. imeripoti kuwa zaidi ya nyumba 550,000 na biashara katika majimbo ya Alabama, Florida na Mississippi ziliachwa bila umeme. Kufikia saa za alasiri, maafisa katika eneo hilo walisema kuwa takriban watu 377 wameokolewa kutoka katika maeneo ya mafuriko na kwamba maafisa 200 wa kituo cha kitaifa cha kukabiliana na vimbunga wangewasili Alhamisi kusaidia katika juhudi ya uokoaji. Maafisa hao pia walitangaza amri ya kukaa majumbani ya siku tatu kuanzia jioni hadi alfajiri katika eneo la Escambia linalojumuisha Pensacola.

USA: Auswirkungen durch Hurricane Sally
Mafuriko yaliosababishwa na Kimbunga Sally jimboni AlabamaPicha: picture-alliance/AP/A. Wang

Kufikia saa za alasiri, kimbunga hicho kilikuwa kimepungua makali na kuwa kama dhoruba ya kitropiki huku kasi ya upepo ikipungua kufikia kilomita 110 kwa saa. Hata hivyo wataalamu wanahofia kutokea kwa uharibifu zaidi katika siku zijazo na mvua ikitarajiwa siku nzima leo Alhamisi.

Afisa mkuu wa usalama katika eneo la Escambia David Morgan amesema maelfu ya raia wengine huenda wakayapa kisogo makaazi yao kutokana na maji yanayoongezeka katika siku zijazo. Morgan ameongeza kwamba kuna baadhi ya jamii zitakazohamishwa kabisa na kwamba itakuwa operesheni kubwa katika siku chache zijazo.

Gavana atangaza hali ya dharura

Magavana wa Mississippi na  Alabama pia wametangaza hali za dharura katika majimbo yao. Akiwahutubia wanahabari, gavana wa Alabama Kay Ivey amesema "tunakabiliwa na mafuriko makali ya kihistoria, maji yanapozidi kupanda, athari ya kupoteza maisha na mali pia inaongezeka.''

Sally ni moja ya vimbunga vitano vya kitropiki ambavyo sasa vinatokea katika Bahari ya Atlantiki, hali ambayo wataalam wa hali ya hewa wanasema imeshuhudiwa mara moja tu hapo awali, mnamo Septemba 1971. Kufikia mwishoni mwa mwezi Agosti, kimbunga Laura kilisababisha uharibu mkubwa nchini Marekani na kuwauwa watu 14 katika majimbo ya Louisiana na Texas. Maelfu ya watu bado wanaishi katika giza kutokana na kimbunga hicho na wengine bado wako katika mahema.

Kimbunga Teddy pia kilitokea katika bahari ya Atlantiki siku ya Jumatano kikikwa na upepo wa kasi ya kilomita 160 kwa saa. Watabiri wa hali ya hewa wanasema huenda kikafikia kiwango cha 4 cha nguvu kabla ya kufikia Bermuda, ambayo siku chache zilizopita ilikumbwa na kimbunga Paulette.

Rais wa Marekani Donald Trump amefananisha kimbunga Sally na kimbunga Laura, lakini amesema dhoruba hiyo ''inadhibitiwa''.