1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kimya cha viongozi wa Kiafrika kwa Gaddafi chakosolewa

4 Machi 2011

Licha ya jumuiya ya kimataifa kusimama pamoja imara dhidi ya kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi, mataifa ya Kiafrika yanajiepusha kuzungumzia lolote kuhusu Libya, jambo ambalo linakosolewa sana.

https://p.dw.com/p/10TOu
Maandamano dhidi ya Gaddafi, Malaysia
Maandamano dhidi ya Gaddafi, MalaysiaPicha: dapd

Gaddafi na Afrika ni maneno ambayo imekuwa ikifanana kwa zaidi ya miaka 40 sasa. Na mwenyewe amekuwa akijichukulia, na kutaka aonekane, kama ndiye mwanajeshi wa Afrika.

"Mimi ndiye kiongozi wa viongozi wote wa Kiarabu, mfalme wa wafalme wote wa Afrika, imamu wa Waislamu wote." Ndivyo alivyosema Muammar al Gaddafi katika mkutano wa Umoja wa Nchi za Kiarabu uliofanyika Qatar mwaka 2009.

Kiongozi huyu mwenye maono yake mwenyewe, hakujijengea himaya ya ubabe ndani tu ya nchi yake, bali kwa karibuni bara zima la Afrika.

Muammar Gaddafi
Muammar GaddafiPicha: picture-alliance/dpa

Kwa zaidi ya miaka 40 amekuwa akifanya mambo kivyake, akiyafadhili makundi ya waasi, lakini wakati huo huo akihimiza kwa vitendo, ndoto ya Afrika kuungana kuwa nchi moja, chini ya jina la Umoja wa Mataifa ya Afrika.

"Ikiwa Gaddafi atakwenda, basi yale matarajio ya Afrika pia yatakwenda pamoja naye. Kwa sababu ni yeye mwenye nishati na rasilimali za kutosha kulitimiza lengo hili la kuifanya Afrika kuwa na hoja imara." Anasema Kabiru Mato, mtaalamu wa sayansi ya siasa wa chuo kikuu cha Abuja, Nigeria.

Ni kutoka kwa Gaddafi ndiko kulikozuka lile wazo la kuwa na huu umoja wa sasa Afrika, kama jumuiya ya mataifa ya Afrika yenye lengo la kufanya kazi pamoja kwa umakini na undani zaidi. Ilikuwa mwaka 2002 jambo hilo lilipowezekana.

Na hili ni kwa kuwa, mbele ya mataifa masikini ya marafiki zake wa Kiafrika, Gaddafi aliyawacha makasha yote wazi. Alifadhili karibuni kila kitu, tangu mabenki, miradi ya maendeleo, ujenzi wa barabara, mahoteli, hadi misikiti.

Kwa hivyo, si jambo la ajabu sana kwamba maraisi wengi wa Kiafrika, wanatoa kauli nyepesi tu panapohusika kile kinachoendelea sasa nchini Libya.

"Tunafadhaishwa sana. Hivyo ndivyo yalivyo mataifa mengi ya Afrika. Lakini kinachotokea Libya, ni jambo ambalo linaweza kutatuliwa kwa majadiliano." Rais wa Msumbiji, Armando Guebuzza

Mtu anaweza kusema pia kuwa hata katika mapinduzi ya Tunisia na Misri, Umoja wa Afrika, ulisema machache sana. Na kwa hili la Libya, ndiyo unasema machache zaidi.

"Kwa hakika viongozi wa Afrika hawataki kuonesha upande gani wanaegemea. Maana hayo hayo yanawakabili wenyewe katika nchi zao. Wito wa demokrasia zaidi na vita dhidi ya ufisadi ni mapambano ya kudumu barani humo. Lakini kwa upande wa Gaddafi, yeye ni mfadhili mkuu barani Afrika, na linapokuja suala la wahamiaji wanaotoka magharibi ya Afrika kuingia Ulaya, ana dhima kubwa sana." Anasema mtaalamu wa masuala ya Afrika katia Taasisi ya Utafiti wa Mambo ya Siasa ya Paris, Philippe Hugon.

Kwa kiasi fulani, namna Libya inavyolishughulikia suala la wahamiaji haramu, kumemugharimu Gaddafi mbele ya uso wa Waafrika wanaopigania kuingia barani Ulaya.

Na askari wa mpakani barani Ulaya hawajaweza kumsaidia kupata mashabiki. Lakini, bado katika makasri mengi ya maraisi, Gaddafi amekuwa akipokewa kiheshima.

Na hadi hapo watakapomgeuka, mfalme huyu wa wafalme, anabakia kuwa mmoja wa waliokalia kiti cha enzi kwa miaka mingi zaidi barani humo.

Mwandishi: Marc Drugge/ZPR
Mhariri: Othman Miraji