1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAfghanistan

Kiongozi wa Afghanistan asema hadhi ya wanawake imebadilika

25 Juni 2023

Kiongozi wa juu wa kidini nchini Afghanistan Hibatullah Akhundzada amesema kwamba wanawake nchini humo "wamekombolewa kutoka kwenye unyanyasaji wa kiutamaduni" baada ya kufuata utawala wa Kiislamu ulio madarakani.

https://p.dw.com/p/4T2JT
Afghanistan Emir der Taliban Mawlawi Hibatullah Akhundzada
Picha: CPA Media Co. Ltd/picture alliance

Ameongeza kuwa hadhi za wanawake nchini humo sasa zimebadilika na kuwafanya wawe viumbe wenye heshima.

Akhundzada ambaye huonekana kwa nadra hadharani, ametoa kauli hiyo wakati wa maadhimisho ya wiki ya sikukuu za Eid al-Adha na kusema kwamba hatua muhimu zinapaswa kufuatwa ili kuboresha hali za wanawake kama sehemu ya jamii. Na kwamba taasisi zote zinapaswa kuwasaidia wanawake kuhakikisha usalama wa ndoa zao, urithi na haki nyinginezo.

Soma pia :UN yaionya Taliban kuhusu haki za wanawake na wasichana

Ameyazungumza hayo ikiwa ni wiki moja tu, tangu Umoja wa Mataifa ulipoelezea wasiwasi wa namna haki za wanawake zinavyokiukwa nchini Afghanistan chini ya utawala wa Taliban.

Tangu utawala huo ulipoingia madarakani, mamlaka nchini humo zimewazuia watoto wa kike na wanawake kuhudhuria masomo ya sekondari au chuo na kuwapiga pia marufuku katika maeneo ya bustani, majengo ya kufanyia mazoezi na kuwataka kujisitiri wanapotoka nyumbani.