Kiongozi wa maandamano Morocco afungwa jela miaka 20
27 Juni 2018Kiongozi mwenye haiba wa vuguguvu lililofanya maandamano nchini Morocco amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela pamoja na wanaharakati wengine watatu baada ya maandamano makubwa ya umma yaliyochochewa na kifo cha mchuuzi mmoja wa samaki.
Nasser ZefZafi na wanaharakati watatu walihukumiwa jana kwa kosa la kutishia usalama wa taifa. Wanaharakati wengine 50 walioshiriki maandamano ya mwaka 2017 ya Hirak Rif walihukumiwa vifungo kati ya mwaka mmoja hadi miaka 15 jela kwa kukutikana na hatia ya makosa madogo.
Kiini cha maandamano hayo kilianzia mwezi October 2016 baada ya mchuuzi masikini wa samaki katika jimbo la BerBer Rif kugongwa na kufa wakati akijaribu kumuokota samaki wake aina ya msuri aliyechukuliwa na polisi na kutupwa kwenye lori la takataka. Zefzafi alikamatwa mwezi Juni 2017 baada ya kutafutwa kwa muda.