1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaCambodia

Kiongozi wa upinzani Cambodia afungwa kwa kosa la uhaini

3 Machi 2023

Kiongozi wa upinzani nchini Cambodia Kem Sokha leo Ijumaa amehukumiwa kifungo cha miaka 27 jela kwa kosa la uhaini, hukumu ambayo imemuondoa kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi mwaka huu.

https://p.dw.com/p/4OCc9
Kambodscha Politik Kem Sokha
Picha: Heng Sinith/AP Photo/picture alliance

Kem Sokha alishtakiwa kwa kula njama na mashirika ya kigeni kwa nia ya kuipindua serikali ya Waziri Mkuu wa muda mrefu Hun Sen, alipokamatwa mwaka 2017.

Sokha, mwenye umri wa miaka 69 na mwanzilishi mwenza wa chama cha kisiasa kilichovunjwa cha Cambodia National Rescue Party CNRP, kwa muda mrefu amekuwa hasimu wa kisiasa wa Hun Sen, ambaye wakosoaji wanasema amerudisha nyuma maendeleo ya kidemokrasia nchini Cambodia na kutumia idara ya mahakama kama silaha ili kukandamiza upinzani.

Soma zaidi:Wakili wa Ujerumani kuwatetea wahanga wa mauaji ya Cambodia

Kiongozi huyo wa upinzani mara kwa mara amekanusha mashtaka dhidi yake, ambayo mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema ni mashtaka ya kubambikiziwa ili kumzuia kushiriki katika uchaguzi wa mwezi Julai mwaka huu.

Mara tu baada ya hukumu katika mahakama ya Phnom Penh kutolewa, Sokha aliwekwa chini ya kizuizi cha nyumbani na kupigwa marufuku kukutana na wageni kutoka nje pamoja na mtu yeyote ambaye sio familia yake bila kibali cha mahakama.

Marekani yaukosoa uamuzi wa mahakama

Belgien | EU ASEAN Gipfel in Brüssel | Rede Hun Sen
Waziri Mkuu wa Cambodia Hun SenPicha: Geert Vanden Wijngaert/AP Photo/picture alliance

Binti yake Kem Monivithya ameandika kwenye mtandao wake wa Twitter kuwa, babake yuko chini ya uangalizi wa polisi. Balozi wa Marekani nchini humo Patrick Murphy, aliyekuwepo mahakamani wakati hukumu hiyo ilipotolewa, ameishtumu hukumu hiyo na kusema ni "ukosefu wa haki.”

Bwana Murphy amewaambia waandishi habari, "Marekani inasikitishwa sana na hukumu ya kiongozi wa kisiasa anayeheshimika Kem Sokha.” 

Soma pia:UN yapitisha azimio la kumalizwa kwa machafuko Myanmar

Agosti mwaka uliopita, Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken alikutana na Kem Sokha wakati wa ziara yake mjiini Phnom Penh, ampapo aliibua wasiwasi juu ya demokrasia inayosuasua chini ya uongozi wa Waziri Mkuu Hun Sen.

Phil Robertson wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch amesema uamuzi huo unaonyesha kile alichokiita, "ushindi wa waimla” nchini Cambodia.

Mwandishi wa shirika la habari la AFP ameripoti kuwa, wakati Kem Sokha alipokuwa akitolewa nje ya mahakama, alionyesha tabasamu na kuwasalimia wanadiplomasia waliohudhuria kikao cha kesi dhidi ya kiongozi huyo wa upinzani.

Sokha ana muda wa mwezi mmoja kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo na kifungo cha jela. Mahakama pia ilimpokonya haki yake ya kupiga kura na kumzuia kuwania nafasi yoyote ya kisiasa.

Chama cha CNRP chavunjwa na mahakama 

Miezi miwili baada ya Kem Sokha kukamatwa mnamo mwaka 2017, mahakama ya juu nchini humo ilikivunja chama cha CNRP, ambacho kwa wakati fulani kilichukuliwa kuwa mpinzani pekee wa chama tawala cha Cambodian People's Party CPP.

Hali hiyo ilifungua njia kwa CPP na Hun Sen kushinda viti vyote 125 vya ubunge mwaka wa 2018, na kuifanya nchi hiyo kuwa ya chama kimoja.

Viongozi kadhaa wa upinzani pia walihukumiwa kwa kosa la uhaini mwaka jana, baadhi hata bila kuwepo mahakamani, katika hatua ya hivi karibuni kuukandamiza upinzani kuelekea uchaguzi.