Kiongozi wa Upinzani Myanmar afunguliwa mashtaka
14 Mei 2009Kiongozi huyo wa upinzani ambaye amekuwa katika kizuizi cha ndani kwa miaka sita sasa anahusishwa na tukio la raia mmoja wa Marekani aliyeingia nyumbani kwa kiongozi huyo bila ya kuruhusiwa na mamlaka husika.
Mwanasheria wa Bibi Aung San Suu Kyi amesema kuwa mteja wake mapema leo amechukuliwa na kupelekwa katika gereza lililoko kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Rangoon, tayari kukabiliwa na kosa hilo.
Raia wa Marekani, John William Yettaw, alikamatwa wiki iliyopita wakati alipokuwa akiogelea kutoka katika makaazi ya kiongozi huyo ambako alikuwa amekaa kwa muda wa siku tatu.
Anatuhumiwa kuogelea na kuvuka ziwa kwa siri kuelekea nyumbani kwa kiongozi huyo wa chama cha National League for Democray.
Lakini mwanasheria wa kiongozi huyo, Kyi Win, amesema mteja wake hakumualika Mmarekani huyo nyumbani kwake ambako amekuwa akitumikia kifungo cha nyumbani kwa miaka sita sasa, kifungo ambacho kinamalizika tarehe 27 mwezi huu.
Kyi Win amesema mwaka jana marekani huyo alijaribu kuonana na Suu Kyi, lakini tukio hilo liliripotiwa katika mamlaka husika baada ya kukaa kuondoka pale alipoombwa kufanya hivyo.
Haijajulikana bado anashtakiwa chini ya makosa gani, lakini wafuatiliaji wa siasa za Myanmar wanasema kuwa huenda akafunguliwa mashtaka chini ya sheria za usalama wa nchi na kukabiliwa na kifungo cha hadi miaka saba gerezani iwapo atapatikana na hatia.
Aung Zauh ni Mhariri wa jarida la Eurowady nchini Myanmar
´´Ni wazi kuwa utawala wa kijeshi wa Myanmar unatafuta uhalali wa kurefusha kifungo chake cha ndani ambacho ilikuwa kimalizike mwezi huu.Kwa hiyo, tubiri kuona atashtakiwa chini ya makosa gani, na ni dhahiri kabisa kuwa huu ni msukumo wa kisiasa kuhalalisha kifungo chake kwa mwaka mmoja zaidi´´
Wanaharakati wa haki za binaadamau wamepinga hatua hiyo ya utawala wa kijeshi wakisema kuwa ni jajribio la kutaka kumzuia asishiriki katika uchaguzi mkuu ambao wakuu wa uatawala huo wameahidi kufanyika mwakani.
Kiongozi wa upinzani nchini Malaysia, Anwar Ibrahim, amesema kuwa Aung San Suu ni nembo ya vuguvugu la demokrasia na uhuru katika eneo la Asia.
´´Tumeona upinzani mkubwa katika eneo hili la Asia na pia ongezeko kubwa la matakwa kutoka katika makundi ya kijamii, na Aung Saan Suu Kyi anaonekana kama nembo ya demokrasia na uhuru katika eneo hili. Ni mwana mama mwenye uwezo na akili, na Myanmar inamhitaji ili kuimarisha uchumi wake na kuiunganisha nchi´´
Aung San Suu Kyi anatarajiwa kupandishwa kizimbani pamoja na raia huyo wa Marekani, halikadhalika daktari wake, Tin Myo Win, ambaye alikamatwa wiki iliyopita kwa kosa kama hilo.
Wiki iliyopita kiongozi huyo wa upinzani nchini Myanmar aliripotiwa kusumbuliwa na maradhi ya msukumo mdogo wa damu pamoja na tumbo la kuendesha, lakini mwanasheria wake anasema kuwa hali yake imeimarika.
Aung San Suu Kyi alikata rufaa kupinga kurefushwa kifungo chake hicho mwaka jana, akisema ni kinyume cha sheria za nchi hiyo.
Mwandishi:Aboubakary Liongo
Mhariri:Othman Miraji