Kiongozi wa upinzani wa Msumbiji atangaza kurejea nyumbani
6 Januari 2025Venancio Mondlane, aliyeondoka Msumbiji baada ya wakili wake kupigwa risasi na kuuawa mnamo Oktoba 19, ameandika kupitia mtandao wa Facebook kwamba atawasili uwanja wa ndege wa Mavalane siku ya Alkhamis.
Akiwa kwenye eneo lisilofahamika, mwanasiasa huyo ambaye anadai kushinda uchaguzi wa Oktoba 9, amewataka wafuasi wake kujitokeza kwa maandamano zaidi.
Soma zaidi: Baraza la katiba laidhinisha matokeo ya uchaguzi Msumbiji
Maandamano hayo yamekuwa yakikabiliwa na ukandamizaji wa polisi, na hadi sasa watu 300 wameshapoteza maisha, kwa mujibu wa takwimu zilizokusanywa na mashirika ya haki za binaadamu.
Mondlane na wafuasi wake wanadai chama tawala cha FRELIMO, ambacho kimekuwapo madarakani kwa miongo mitano sasa, kiliiba uchaguzi wa Oktoba 9, baada ya Tume ya Uchaguzi kumtangaza mgombea wake, Daniel Chapo, kushinda kwa asilimia 65, na kumpatia Mondlane asilimia 24.