1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa upinzani wa Myanmar Aung San Suu Kyi aachiliwa huru

Oumilkher Hamidou15 Novemba 2010

Matumaini ya umma baada ya kuachiwa huru kiongozi wa upande wa upinzani na mshindi wa zawadi ya amani ya Nobel Aung San Suu Kyi

https://p.dw.com/p/Q8bp
Mpenda mageuzi ya kidemokrasi Aung San Suu Kyi akiwahutubia wafuasi wakePicha: AP

Kiongozi wa upinzani Aung San Suu Kyi anaeunga mkono demokrasia nchini Myanmar ametoa hotuba yake kuu ya kwanza, siku moja tu baada ya kuachiliwa huru.Katika hotuba yake hiyo siku ya jumapili, aliwahimiza maelfu ya wafuasi wake kugombea demokrasia na haki zao. Je,kwa umbali gani mshindi huyo wa Tuzo ya Amani ya Nobel ni kitisho kwa utawala wa kijeshi nchini humo na atakuwa na uhuru gani wa kisiasa?

Wafuasi wa Aung San Suu Kyi walimshangiria kiongozi huyo wa upinzani alipojitokeza kwa muda mfupi mbele ya nyumba yake siku ya Jumamosi, baada ya kumaliza kifungo chake cha mwisho cha miaka saba. Wafuasi hao na waandishi wa habari walikusanyika nje ya geti la nyumba yake. Mshindi huyo wa Tuzo ya Amani ya Nobel, aliekuwa kizuizini miaka 15 kutoka 20 iliyopita, aliumbia umati huo kuwa amefurahi kuona jinsi alivyokaribishwa na kuungwa mkono. Akijaribu kuutuliza umati uliokuwa ukimshangiria alisema, wakati wa kupaza sauti utakuja na utakapowadia, wala wasibakie kimya.

Siku ya Jumapili mjini Yangon akatoa hotuba yake kuu ya kwanza katika makao makuu ya chama chake "Umoja wa Kitaifa kwa Demokrasia" NLD. Katika hotuba hiyo,aliwahimiza wafuasi wake kugombea demokrasia na haki zao. Amesema, demokrasia ipo pale serikali inapodhibitiwa na umma. Demokrasia ni kuwepo uhuru wa kueleza maoni. Akauambia umati huo kwamba anataka kushirikiana na makundi yote ya kidemokrasia. Vile vile angependa kusikia maoni ya umma na baadae wataamua cha kufanywa. Chama chake cha NLD, kilishinda uchaguzi wa mwaka 1990 kwa uwingi mkubwa lakini utawala wa kijeshi ulikataa kuheshimu matokeo hayo. Mwaka huu, chama hicho kilikitaa kushiriki katika uchaguzi wa Novemba 7 na kikavunjwa na utawala wa kijeshi. Uchaguzi huo wa kwanza kufanyika nchini Myanmar baada ya miaka 20, umekosolewa na makundi ya haki za binadamu na nchi za magharibi kama ni njama ya kurefusha utawala wa kijeshi nchini humo.

Aung San Suu Kyi Unterstützer feiern vor ihrem Haus
Wafuasi wa kiongozi wa upinzani wakimshangiria mbele ya nyumba yakePicha: AP

Kwa maoni ya wachambuzi wa kisiasa,utawala wa kijeshi bado unamuona Suu Kyi kama ni tishio kwa sababu ya umaarufu wake mkubwa. Balozi wa zamani wa Uingereza nchini Thailand Derek Tonkin alie mchambuzi maarufu wa masuala ya Myanmar amesema, Suu Kyi anaweza kuwa na umuhimu mkubwa ikiwa atapewa fursa hiyo. Viongozi wa kimataifa wamefurahia kuachiliwa huru kwa Suu Kyi, lakini pia wameuhimiza utawala wa kijeshi kuwaachilia huru wafungwa wa kisiasa ikikadiriwa kuwa wanafikia 2,100. Waziri wa masuala ya nchi za nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle amesema:

"Tunatazamia kuwa kuachiliwa huru kwake ni hatua ya mwanzo. Bado kuna wafungwa wengi wa kisiasa.- wao pia wanapaswa kuachiliwa huru moja kwa moja."

Suu Kyi mwenye miaka 65,huenda akaipa nguvu mito ya demokrasia nchini Myanmar.Wanadiplomasia wanamtazamia Suu Kyi kushirikiana na nchi za magharibi ili kuondoa vikwazo alivoviunga mkono hapo awali kwani wengi wanaamini vikwazo hivyo vinawaathiri wananchi na sio utawala wa kijeshi. Myanmar yenye wakaazi milioni 50 na utajiri wa maliasili ni miongoni mwa nchi zilizotopea kwa rushwa duniani. Kiasi ya theluthi moja ya umma unaishi katika hali ya umasikini mkubwa.

Mwandishi: Martin,Prema/RTRE/DPAE

Mpitiaji: Abdallah,Maryam