1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafaransa watakiwa waamue

13 Desemba 2015

Chama cha Front National-FN,kinategemea kuibuka na ushindi katika duru ya 2 ya uchaguzi wa majimbo,katika zoezi hili muhimu la uchaguzi kabla ya uchaguzi wa rais mwaka 2017 dhidi ya mrengo wa shoto na wahafidhina.

https://p.dw.com/p/1HMcw
Rais Francois Hollande akipiga kura katika duru ya pili ya uchaguzi wa majimboPicha: Reuters/R. Duvignau

Hatima ya uchaguzi huu wa duru mbili uliogubikwa na mashambulio ya kigaidi ya Novemba 13 mjini Paris ambapo watu 130 waliuwawa,haijulikani. Itategemea na idadi ya wapiga kura na jinsi wapiga kura wa mrengo wa kushoto watakavyoelemea upande wa wahafidhina ili kuwafungia njia FN na kiongozi wao Marine Le Pen wasishinde katika majimbo kadhaa ya nchi hiyo.

Vituo vya kupiga kura vimefunguliwa tangu saa nne asubuhi kwa saa za Afrika mashariki,mbili kwa saa za ulaya ya kati.Hatua za usalama zimeimarishwa katika vituo vya kupigia kura na hasa katika mji mkuu Paris. Wapiga kura milioni 45 na laki tatu wanatarajiwa kuteremka vituoni katika zoezi hili la kupiga kura linalofanyika chini ya hatua za hali ya dharura.

Katika duru ya kwanza ya uchaguzi decemba 6 iliyopita,mpiga kura mmoja kati ya wawili,na thuluithi mbili ya vijana wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi 24 walionesha kutoridhika kwao na hali namna ilivyo nchini na kwa namna hiyo kususia vituo vya kupiga kura.

Vyama asilia vya kisiasa vinalaumiwa kutoutambua ukweli wa mambo

"Ulimwengu wa kisiasa unashindwa kuitambua hali namna ilivyo" anasema Sylvain,mwenye umri wa miaka 34 na kuongeza;"kuwataka watu wakapige kura ili kuwazuwia FN,bila ya viongozi wenyewe kutafakari japo kidogo ni ushahidi kwamba kuna tatizo kubwa huku."

Frankreich Zweite Runde der Regionalwahlen 2015 Marine Le Pen
Mwenyekiti wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia Front National,Marine Le PenPicha: Reuters/P. Rossignol

Kudhibitiwa jimbo moja au zaidi na chama cha siasa kali za mrengo wa kulia litakuwa tukio la kwanza la aina yake nchini Ufaransa ambako FN na hotuba zake zilizojaa chuki dhidi ya wahamiaji na dhidi ya Umoja wa ulaya wanazidi kujipatia umashuhuri kila uchaguzi unapaoitishwa tangu miaka mitano iliyopita-wakifaidika kwa kero za wananchi dhidi ya kushindwa vyama asilia kuushughulikia mzozo wa kiuchumi.

Katika duru ya kwanza,chama cha Marine Le Pen kilivunja rikodi kwa kujikingia karibu asili mia 28 ya kura na kukmata nafasi ya mwanzo ya matokeo katika majimbo sita kati ya 13 yanayogombaniwa. Mhula madarakani ni wa miaka sita.

Katika raundi ya pili,angalao jimbo moja linaonyesha "ni hakika litadhibitiwa na FN" anaashiria Jean-Daniel Lévy wa taasisi ya utafiti wa maoni ya wananchi "Harris Interactive." Hadi majimbo matano yanaweza kudhibitiwa na FN" anaashiria kwa upande wake Bruno Jeanbart wa taasisi ya OpinionWay.

Nafasi nzuri ya ushindi kwa FN inaweza kuwa katika eneo la mashariki ya Ufaransa (Alsace,Champagne-Ardennes Lorraine). Eneo la kati mashariki,La Bourgogne-Franche-Comté lnaonyesha pia huenda likaangukia upande wa FN.

Matumaini ya Nicolas Sarkozy ya kurejea Elysée yanaonyesha kufifia

Waziri mkuu Manuel Valls amezungumzia kitisho cha "Vita vya wenyewe kwa wenyewe" pindi FN wakiingia madarakani. Marine Le Pen ameahidi "kuvuruga shughuli za serikali" pindi wakishinda katika eneo la kaskazini.

Frankreich Wahlen Nicolas Sarkozy
Mwenyekiti wa chama cha kihafidhina Republican-Nicolas SarkozyPicha: Reuters/E.Feferberg

Matokeo ya chaguzi za majimbo yanapewa umuhimu mkubwa kulekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2017-kwasasa Marine Le Pen anaongoza utafiti wa maoni ya wapiga kura.

Hali hiyo itazidi kudhoofisha matumaini ya rais wa zamani Nicolas Sarkozy anaekabiliana na wapinzani wawili ndani ya chama chake cha Republican-mawaziri wakuu wa zamani,Alain Juppé na Francois Fillon.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri : Isaac Gamba