1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kishindo cha Obama Care cha muelemea rais Donald Trump

Oumilkheir Hamidou
19 Julai 2017

Kushindwa rais wa Marekani Donald Trump kuifuta "Obama Care, hatua za aina gani zichukuliwe dhidi ya Uturuki na kashfa ya vijana wa kwaya katika kanisa la mjini Regensburg "Domspatzen" ni miongoni mwa mada magazetini

https://p.dw.com/p/2gmc1
Obama Care Obamacare USA medizinische Versorgung
Picha: Getty Images/J.Moore

 

Tunaanzia Marekani ambako miezi sita baada ya kuingia madarakani rais mpya Donald Trump, ahadi kubwa aliyoapa kuitekeleza mara baada ya kuingia madarakani, yaani  kuifuta katika madaftari ya historia bima ya afya iliyoanzishwa na mtanagulizi wake, ObamaCare, ameshindwa kuibadilisha. Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linaaandika: "Kushindwa mpango wa rais Trump wa kuifanyia marekebisho bima ya afya si chochote chengine isipokuwa kushindwa utawala wake. Nafasi ya marekebisho baada ya mapumziko ya msimu wa joto ni finyu. Mazungumzo ya shida yanaonyesha si mikato ya rais huyo wa Marekani. Siri ya ufanisi wake ni kufanya kila liwezekanalo, hata katika hali ya shida aonekane hakuna kama yeye na ikilazimika hata kwa kutoa hoja zisizokuwa na msingi. Kutokana na purukushani ukweli pengine hautafichuliwa. Huo ndio mtindo aliouzowea na anaoudhibiti kikamilifu na hadi wakati huu amefanikiwa. Ingawa umashuhuri wake kwa jumla umepungua , hata hivyo wafuasi wake bado wanaendelea kumuunga mkono. Wanatambua si kiongozi mzuri lakini ni wao.

Nini cha kufanya kumzindua Erdogan?

Uturuki inazidi kugonga vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani. Baada ya kuwaandama waandishi habari, sasa serikali ya rais Recep Tayyip Erdogan inawageukia wanaharakati wa haki za binaadam. Gazeti la "Freie Presse" linajiuliza hatua za aina gani zinafaa kuchukuliwa ili kuitanabahisha Uturuki irejee katika njia ya maana? Eti ndo kusema vikwazo vya kiuchumi vuizidishwe makali, kwa mfano kwa kusitishwa mazungumzo ya kujiunga na umoja wa forodha? Lakini kwa kufanya hivyo viongozi wa mjini Ankara, watawapata washirika wengine, baada ya muda mfupi au mrefu unaokuja. Hatua kali za Ujerumani zina kikomo pia. Erdogan anaweza wakati wowote ule kusema anabatilisha makubaliano yaliyofikiwa pamoja na Umoja wa ulaya kuhusu wakimbizi. Hilo ni jinamizi kubwa. Ulaya inakabiliwa na changamoto ambayo hakuna anaejua mwisho wake. Kwa hivyo rais wa Uturuki ndie anaeshikilia turufu zote mkononi mwake. Kwasababu hata jumuia ya kujihami ya NATO inaihitaji Uturuki. Na Erdogan anaonyesha amedhamiria kufuata njia aliyojichorea. Waturuki wengi wanampenda kwasababu hiyo hiyo. Ulaya haina njia isipokuwa kukodowa macho.

Kashfa ya Regensburger Domspatzen

Mada yetu ya mwisho inahusu kashfa iliyoanza tangu mwaka 1945 katika kanisa kuu la mjini Regensburg ambako vijana wa kwaya-"Domspatzen" waliteswa na kudhalilishwa na baadhi ya viongozi wa kanisa hilo. Gazeti la  "Allgemeine Zeitung" linaandika:"Kanisa limekawia sana kuchunguza kashfa hiyo na kutambua makosa yaliyofanyika. Kuna waliokuwa wakituliza mambo na wengine wakiyafifiisha. George Ratzinger, nduguye kiongozi wa zamani wa kanisa katoliki ulimwenguni, anatuhumiwa kuyafumbia macho yaliyotokea. Jambo hilo linatisha. Na pale kiongozi wa kanisa la Regensburg anaposema "walistahiki kuwa waangalifu zaidi zamani" basi maneno hayo ni sawa na kumkaripia askofu mkuu wa kanisa la kuu la Regensburg kardinali Müller wa kutoka Mainz.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlanadspresse

Mhariri:Josephat Charo