Kishindo cha uchaguzi mkuu nchini Ujerumani
25 Septemba 2013Tuanzie lakini na juhudi za kuunda serikali ya muungano. Manung'uniko yanakutikana kila upande miongoni mwa vyama vinavyoweza kuwa na nafasi ya kushiriki katika serikali ya muungano. Gazeti la "Rhein-Neckar-Zeitung" linaandika:"Sawa na SPD na wanachama wa muungano wa CDU/CSU pia wanaridhia shingo upande kuundwa serikali ya muungano pamoja na SPD. Haitasaidia pakubwa, ikitengwa ile hali ya kudhihirisha misuli ya vyama vikuu dhidi ya mbilikimo wa kisiasa. Ukipiga hesabu na hasa ukitanguliza mbele muundo madhubuti wa bunge lenye wingi wa viti kwa vyama vinavyounda serikali na wakati huo huo lenye kudhamini upande wa upinzani wenye nguvu, basi mtu anaweza kusema kuna njia bora zaidi ya kuunda serikali ya muungano; nayo ni kati ya CDU/CSU na walinzi wa mazingira."
Matokeo yasiyokadirika ya uchaguzi mwengine
Kansela Angela Merkel ana jumla ya siku 30 kuunda serikali, akishindwa, uchaguzi mkuu mpya utabidi uitishwe. Gazeti la "Lausitzer Rundschau" linaandika:"Wakishindwa kuungana na kumchagua kansela, basi uchaguzi mpya ndio itakayokuwa njia pekee ya kujikwamua. Spika wa bunge atabidi alivunje bunge. Hali hiyo sio tu itadhoofisha hadhi ya uaminifu ya Ujerumani barani Ulaya, lakini pia mtu hatohitaji kuonyeshwa ruuya kuweza kujua matokeo ya uchaguzi huo yatakuwa ya aina gani:muungano wa vyama ndugu vya CDU/CSU wa kansela Angela Merkel ukiachwa mkono na SPD na walinzi wa mazingira die Grüne, vinaweza kutegemea kujikingia wingi mkubwa kabisa wa kura. Au pengine hata FDP wakafufuliwa tena na wapiga kura na kuendeleza kwa namna hiyo muungano uliokuwepo hadi sasa kati ya CDU/CSU na waliberali. Njia zote hizo mbili, SPD na die Grüne wasingezipendelea - kwa sababu kwao wao hilo lingekuwa pigo kubwa zaidi kuliko lile la Jumapili iliyopita, Septemba 22."
Walinzi wa mazingira serikalini?
Gazeti la "Sächsische Zeitung" linatafakari hali namna ilivyo ndani ya chama cha walinzi wa mazingira die Grüne na kuandika:"Hali ndani ya chama cha kijani ni tete zaidi. Chama hicho hakikuyafikia hata kidogo malengo yake katika uchaguzi mkuu uliopita. Wanabidi sasa watafakari makosa yaliyofanyika, wabadilishe uongozi ili waweze kuchipuka. Ni sawa kabisa kwamba mazungumzo pamoja na CDU/CSU yatakuwa magumu, kinyongo cha kampeni za uchaguzi hakijamalizika na chama chenyewe kinakabwa na mitihani. Lakini hali kama hiyo inakikumba pia chama cha SPD. Walinzi wa mazingira, licha ya huzuni, wanabidi wajiulize kama wataisidia kweli nchi hii wakiamua kushiriki serikalini au kama mzigo huo watawaachia wengine waubebe. Kuzungumzia uwezekano wa kuunda serikali pamoja na kansela Merkel ni jambo la maana na litasaidia kukirejeshea chama hicho hadhi iliyowaponyoka. Lakini wenyewe hawaonyeshi kuutilia maanani uwezekano huo."
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Josephat Charo