Kivumbi chatazamiwa katika mkutano mkuu wa ANC
28 Juni 2017Chama cha ANC kitaanza mkutano wake Ijumaa ya hapo kesho kujadili mwelekeo wa chama mkutano ambao unategemewa kuendelea kugubikwa na mivutano ya ndani kuhusiana . Chama hicho cha ANC kimeshuhudia kashfa chungu nzima za rushwa zinazomuandamana rais Jacob Zuma.Yamekuwa yakifanyika maandamano nchini Afrika Kusini kumshinikiza rais Zuma aliyepoteza umaarufu kujiuzulu. Yote hayo yamekuwa yakifanywa na upinzani unaodai rais Zuma amepoteza uhalali, na huku nazo kura za kutokuwa na imani nae zikigonga mwamba bungeni.Pamoja na hayo wasiwasi wa kuwepo mivutano zaidi ndani ya chama hicho tawala umeongezeka huku pia umaarufu wa chama hicho ukizidi kuporomoka.
Wasiwasi waendelea ndani ya ANC
Chama hicho kinafanya mkutano wake huo wa kisiasa siku ya ijumaa kikiwa katika mazingira hayo ya wasiwasi.Wajumbe elfu tatu watashiriki kikao hicho kitakacho endelea kwa siku tano kujadiliana kuhusu mwelekeo wa chama hicho. Ajenda kuu zitakazo jadiliwa na wajumbe hao zitajikita hasa katika maswala yanayohusu mageuzi kwenye mpango wa kijamii na uchumi. Ukosefu wa ajira nchini Afrika Kusini umefikia asilimia 27.7 ikiwa ni kiwango kikubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa huku pia hali ya kiuchumi katika robo ya kwanza ya mwakaikiwa imeporomoka kwa 0.7 asilimia.Kwa maneno mengine taifa hilo la Afrika Kusini limeshaingia katika mporomoko wa kiuchumi.Sambamba na hayo chama cha ANC kimeshapoteza misingi yake na juu ya hilo hata imani ya wananchi inazidi kupungua. Hii imetokana na hali iliyoshuhudiwa kwenye matokeo ya uchaguzi pamoja na kukosolewa waziwazi chama hicho amesema Jeff Rabete ambae ni waziri katika ofisi ya rais kabla ya mkutano huo. Viongozi kama Rabete wanahisi mjadala kuhusu rais Zuma unaonyesha ni jinsi gani chama hicho kinavyozidi kugawika.Mkutano huo kwa hakika unataka kutafuta njia ya kukiunganisha. Chama hicho, kilichoongoza mapmbano ya ukombozi dhidi ya sera ya kibaguzi Apartheid, i kinataka kutumia swala la kufanyika mageuzi ya kiuchumi kuwavutia wapiga kura zaidi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2019.Na hapo rais Zuma atakuwa amefikia mwisho wa muhula wake wa pili madarakani.Mkutano huo mkuu kwa mujibu wa wachambuzi kama Daniel Silke ndio utakaotoa sura halisi ya maamuzi yatakayofanyika katika mkutano mkuu wa chama mwezi Desemba kuhusu nani atakiongoza chama hicho baada ya Zuma. Mchambuzi huyo akizunguma za DW amesema mkutano huo pia utatoa mwelekeo kuhusu mpango mzima wa chama hicho ikiwa kitafwata mkondo wa kizalendo na siasa kali au kunyamaziana zaidi na kuwepo uwazi.Tayari ilani ya ANC inaonyesha kutaka kupendelewa zaidi kwa waafrika weusi. Hata hivyo Makamu wa rais Cyril Ramaphosa ameonekana kulizungumzia swala hilo kwa uwangalifu akisema ni bora misingi ya uwazi izingatiwa kama inavyoelezwa katika ilani inayohusiana na swala zima la uhuru.
Ikumbukwe kwamba rais Jacob Zuma amekuwa akikosolewa sana kuhusiana na kashfa za rushwa pamoja na uhusiano wake na familia tajiri na maarufu ya kihindi ya Ghupa,na kwa maana hiyo basi mchambuzi Daniel Silke anasema chama hicho cha ANC kinatarajia baada ya Zuma kuondoka itakirudishia heshima na imani miongoni mwa wafuasi wake na wapiga kura.